Friday, August 08, 2014

JIJI LA ARUSHA NA MBEYA KURINDIMA SIFA JUMAPILI HII



JIJI LA ARUSHA NA MBEYA KURINDIMA SIFA JUMAPILI HII

Baada ya kusubiri kwa muda mrefu video ya toleo la 'Nisamehe' hatimaye kwaya kongwe ya Tumaini Shangilieni kutoka kanisa la Mtakatifu James lililopo Kaloleni jijini Arusha, imekamilisha video hiyo na inatarajiwa kuwekwa wakfu rasmi jumapili hii, katika ibada zitakazofanyika katika kanisa lao.

Video hiyo iliyotakiwa kutoka mapema mwaka huu lakini ilishindikana kutokana na kwaya hiyo kutaka kuifanyia marekebisho ili kukutana na kile ambacho watu wanakitarajia kupitia uinjilisti wa kwaya hiyo. Mpaka sasa Tumaini ina matoleo manne ya video na toleo jipya litakalozinduliwa jumapili linaongeza idadi ya kuwa na jumla ya matoleo matano. Kazi kwenu mtakao kuwa jijini Arusha jumapili hii, msisahau kufika Kaloleni St James.


Wakati huohuo baada ya kimya cha muda mrefu cha takribani miaka 10 toka watoe toleo lao linalofanya vizuri mpaka leo liitwalo 'Tunaishi', kwaya ya uinjilisti Forest ya kanisa la Kilutheri Forest jijini Mbeya inatarajiwa kuzindua album tatu mpya za sauti kwa mpigo jumapili hii katika usharika wao wa Forest wakisindikizwa na kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama ya jijini Dar es salaam pamoja na vikundi vingine vya jijini Mbeya.


Kwaya hiyo ilikuwa kimya kwa muda mrefu zamani ilikuwa ikijulikana kama kwaya ya Vijana nasasa Uinjilisti, kati ya nyimbo zao zilizosikika vyema kutoka katika album iliyopita ya 'Tunaishi', wimbo uitwao 'Wewe Mungu' ulitokea kuonyeshwa kila asubuhi katika runinga ya EATV na watu wengi kubarikiwa na ujumbe uliopo kwenye wimbo huo na nyimbo nyingine zilizokamilisha album hiyo ambayo hata hivyo inapatikana mikononi mwa kwaya husika baada ya kuiondoa kwa msambazaji wao.


Tembelea ukurasa wao wa Uinjilisti Forest kwa taarifa zaidi.