Tuesday, March 29, 2016

UKOSEFU WA MADAWATI MKOANI MANYARA MWISHO APRIL 30,2016-DKT JOEL BENDERA



UKOSEFU WA MADAWATI MKOANI MANYARA MWISHO APRIL 30,2016-DKT JOEL BENDERA
Na Woinde Shizza,Manyara.

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera amewaagiza viongozi wa Wilaya za mkoa huo, kuhakikisha hadi mwisho wa mwezi Aprili kusiwepo na wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati ya kukalia.

Akizungumza mjini Babati, Dk Bendera alisema japokuwa Rais John Magufuli amewaagiza wakuu wote wa mikoa kuondoa tatizo la ukosefu wa madawati hadi Juni 30 mwaka huu, kwa Manyara mwisho ni Aprili 30. 

Alisema Manyara haipaswi kusubiri hadi mwezi Juni 30 ili imalize upungufu wa madawati hivyo, wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji, wenyeviti wa halmashauri, viongozi na wananchi kwa ujumla kuhakikisha hilo linafanyika. 

"Rais wetu Dk Magufuli baada ya kututeua hivi karibuni alituagiza wakuu wote wa mikoa kuhakikisha tunamaliza tatizo hilo hadi mwezi wa sita lakini mimi nataka kwangu Manyara ikifika mwezi wanne tumalize," alisema Dk Bendera.

Kwa upande wake, katibu tawala wa mkoa huo Eliakim Maswi alisema kiwango cha elimu Manyara kimeporomoka kwa kuchangiwa zaidi na tabia ya wafugaji kuhama kutoka eneo moja hadi jingine kufuata malisho mazuri ya mifugo yao.

"Hali ni mbaya kwenye halmashauri zetu zenye wafugaji wengi kwani mkoa wetu umeendelea kuporomoka kuanzia ngazi ya elimu ya msingi na sekondari hivyo jitihada za dhati za kupambana na hili zinahitajika," alisema Maswi.

Hata hivyo, aliwataka viongozi wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha shule zote za sekondari ambazo hazijamaliza ujenzi wa vyumba vya maabara, wanamaliza haraka iwezekanavyo ili wanafunzi wapate elimu kwa njia ya vitendo.