Na Woinde Shizza alivyotembelea ,Mwanza .
Uvuvi haramu wa kutumia sumu kali,pamoja na neti umekua ukitishia uhifadhi katika hifadhi ya Taifa ya Saa Nane na Lubondo ambazo zimepewa jukumu la kulinda mazalia ya samaki ili samaki hao wasipotee kwenye uso wa dunia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake waliofanya ziara ya kutembelea hifadhi hiyo ya Saa Nane iliyoko jijini Mwanza ,ziara iliyoratibiwa na Tanapa Mhifadhi Mkuu Donatus Bayona amesema kuwa changamoto inayowakabili ni uvuvi haramu na uvamizi wa maeneo ya hifadhi unaofanywa na wavuvi wanaojipatia kipato bila kujali kuwa wanaharibu mazalia ya samaki .
Askari Wanyamapori katika hifadhi hiyo Aloyce Mong`ee amesema kuwa wamekua wakiimarisha doria katika mipaka ya hifadhi ili kuzuia shughuli hizo za uvuvi ambazo ni tishio kwa uhifadhi."Kuna mipaka ambayo tumeweka hakuna mtu anayeruhusiwa kufanya uvuvi ndani ya eneo la hifadhi ili kuhifadhi mazalia ya samaki" Alisema Askari huyo.
Mhifadhi huyo amesema kuwa Hifadhi hiyo ambayo iko katikati ya jiji la Mwanza inaongoza kwa kuwa na watalii wengi wa ndani ambao ni asilimia 90% ya wageni wanaotembelea hifadhi hiyo.Alisema Hifadhi ya Saa Nane ni moja kati ya hifadhi zilizopo kati kati ya miji hivyo kuvutia watanzania wengi kutembelea eneo hilo ambali lina wanyama pori pundamilia,swala na sokwe weusi pamoja na madhari nzuri na maridhawa ambazo hutumika kama sehemu ya kujifunzia na kupumzikia.