Saturday, December 05, 2015

HAKIELIMU YAMZIMA RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE



HAKIELIMU YAMZIMA RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE
TAASISI isiyo ya kiserikali ya HakiElimu leo imezindua ripoti iliyobainisha madudu yaliyofanywa katika utawala wa Awamu ya Nne chini ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Ndani ya ripoti hiyo iliyobeba miaka 10 ya utawala wa Rais Kikwete sekta ya elimu, imeeleza kuwa katika uongozi wake, ubora wa kiwango cha elimu uliporomoka kuliko wakati mwingine wowote katika histolia ya Tanzania.
Katika ripoti hiyo ambayo iliandaliwa na jopo la wataalamu na wadau wa elimu mbalimbali ambao walifanya katika mwezi Julai na Agosti mwaka huu, pia imebaini utekelezaji hafifu wa ahadi zake alizokuwa akizitoa kwenye sera zake kuhusu uboreshaji wa sekta ya elimu.
Akichambua ripoti hiyo baada ya kuzinduliwa na Mwenyekiti wa Bodi HakiElimu, Martha Qorro, Mhadhili wa Chuo Kikuu Dar es Salaam Prof. Kitila Mkumbo amesema, katika utafiti huo pia walibaini kuwa, Rais Kikwete hakuongeza vitu vipya katika uongozi wake kuhusu sekta ya elimu bali aliendeleza yale aliyoachwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
"Hakuwa na falsafa mpya katika sekta ya elimu bali alichokuwa anafanya ni kuyabeba kila anayoyapata kama yalivyo na kuanza kufanyia kazi.
"Mfano; alisema ataanzisha shule za kimataifa nchini lakini hizo hizo alizoziongeza ndio zipo hoi, hadi sasa shule zenye viwango vinavyokubalika nchini ni asilimia nne tu," amesema Mkumbo.
Mkumbo amesema, alichofanikiwa Rais Kikwete katika uongozi wake ni kupanua fursa za elimu ambapo aliweza kuongeza miundombinu kwa kuongeza madarasa, matundu ya vyoo, kuongeza idadi ya walimu, vitabu, udahili, uwiano kati ya wasichana na wavulana wanaojiunga na shule ya msingi na sekondari lakini sio katika suala la ubora wa elimu.
"Mathalani, shule za msingi zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,538 mwaka 2015 huku wanafunzi wa shule za msingi wakiongezeka kutoka 7,541,208 hadi 8,202,892, shule za sekondari zimeongezeka kutoka 1,745 mwaka 2005 hadi 4,753 mwaka 2015 huku idadi ya wanafunzi shule za sekondari zikiongezeka 524,325 mwaka 2001 hadi 1,804,056 mwaka 2015.
"Vyuo vya ufundi pia vimeongezeka kutoka 184 mwaka 2005 hadi 744 mwaka 2015 huku idadi ya wanafunzi katika vyuo ikiongezeka kutoka 40,059 hadi 145,511 mwaka 2015. Licha ya wanafunzi kuonekana kuwa wengi shuleni na vyuoni, tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonesha wanafunzi wengi hawajui kusoma wala kuandika," amesema Mkumbo.
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage akisoma mapendekezo yaliyopo kwenye ripoti hiyo amesema kuwa, serikali iliyopo madarakani hivi sasa inatakiwa kuchukua maoni yaliyopendekezwa kwenye ripoti hiyo na kuyafanyia kazi ili kuboresha sekta ya elimu nchini.
Akitaja baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo Kalage amesema, serikali ya Awamu ya Tano inatakiwa iwatazeme walimu kwa jicho lingine.
Ili elimu iwe bora lazima walimu pia wawe bora na sio bora walimu hivyo iunde bodi ya kuwachunguza walimu labla ya kuanza kazi kama ilivyo kwa madaktari baada ya kumaliza masomo.
Amesema mapendekezo mengine ni kuwajali walimu ili wapate moyo wa kufanya kazi hiyo kwa kuwajengea nyumba kwani ni asilimia 22 tu ya walimu ndio wamepewa nyumba na kuboresha mioundombinu katika mazingira wanayoishi. Kuboresha madarasa, vifaa vya kufundishia, ukaguzi kwa walimu na mazingira ya shule yaimarishwe.
"Ni kazi ya Rais John Magufuli sasa kuiboresha sekta ya elimu kwani hiyo ndio sekta muhimu na kubwa kuliko zote na ndiyo yenye bajeti kubwa kuliko zote lakini utendaji wake ni ziro sasa hiyo bajeti inaendaga wapi?
"Walimu mishahara haiboreshwi, wanafunzi wengi hawajui kusoma wanamaliza shule kichwani hakuna kitu," amesema Kalage.