Kocha mkuu wa timu ya Taifa 'Taifa Stars' Charles Boniface Mkwasa (kushoto) (kulia) kocha msaidizi Hemed Morocco
Baada ya TFF kuridhia timu ya Taifa kwenda kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Nigeria, benchi la ufundi la Taifa Stars linatarajia kutangaza kikosi siku mbili zijazo kwa kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za AFCON.
Kocha wa timu ya taifa Charles Boniface Mkwasa amesema amefurahishwa na TFF kukubali ombi lake na sasa watakwenda nchini Uturuki kwa kambi ya wiki mbili ambako watapata mechi mbili za kujipima nuvu kabla ya kuivaa 'The Super Eagles'
"Bado kidogo lakini ndani ya siku mbili hizi tutatangaza kikosi, kuna vijana tumewaona kwenye mashindano ya Kagame lakini hatutobadilisha sana ila kuna vijana tumewaona wameonesha viwango vizuri tutajaribu kuwapa nafasi", amesema MKwasa.
"Nimepokea kwa furaha baada ya kusikia ombi letu la kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi limekubaliwa kawasababu cha msingi ni kwamba licha tu ya kusafiri kwenda kuona mazingira lakini kuna mechi za kimataifa ambazo tayari tumeshazipata kwahiyo nadhani itatusaidia kuliko hata tukifanya mazoezi hapa nyumbani".
"Kuna timu ambazo nazo kwa kipindi hicho zinakwenda pale kufanya mazoezi kwahiyo wale maajenti wetu tuliwaambia kwamba tunataka mechi mbili na mechi moja tutacheza na timu ya Libya nadhani itakuwa tarehe 27 na nyingine kama sikosei ni kati ya timu ya Kuwait au Qatar mojawapo lakini siwezi kuconfirm".
Stars inatarajiwa kuvaana na Nigeria kwenye mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mchezo utakaochezwa Septemba 5, kwenye uwanja wa taifa.