Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad
Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad amesema ameshangazwa na sababu zilizotolewa na Profesa Ibrahim Lipumba aliyejivua uenyekiti wa chama hicho, kuwa amechukizwa na kitendo cha kukaribishwa kwa makada wa CCM ndani ya Ukawa.
Akizungumza na wanachama wa CUF makao makuu ya chama hicho Buguruni, Dar es Salaam juzi usiku, Maalim Seif alimtakia kila la kheri profesa huyo mtaalamu wa masuala ya uchumi na kusisitiza kuwa chama hicho kitaendeleza malengo ya kuanzishwa kwake, ikiwa ni pamoja na kushika dola.
Profesa Lipumba, mmoja wa waasisi wanne wa Ukawa-Umoja wa Katiba ya Wananchi unaoundwa na vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi alichukua uamuzi huo juzi na kwamba amejitahidi kuvumilia ujio wa makada wa CCM ndani ya Ukawa, lakini ameshindwa.
Wengine walioongoza harakati za kuasisi Ukawa ni Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Emmanuel Makaidi wa NLD.
Profesa Lipumba, mmoja wa wenyeviti wanne wa Ukawa na mwenyekiti wa wenyeviti hao, aliyeeleza sababu za kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwenye umoja huo takribani siku 10 zilizopita, amejivua wadhifa huo kutokana na vyama hivyo kukubali kupokea watu walioshiriki kukataa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na wananchi, kitu ambacho kilikuwa msingi wa kuundwa kwa Ukawa.
"CUF kipo imara na katika mikono salama kabisa. Mimi na viongozi wenzangu tuliobaki tutahakikisha chama hiki kinafikia malengo ya kuundwa kwake, hakuna jingine isipokuwa kukamata hatamu ya dola," alisema Maalim Seif na kushangiliwa na kundi kubwa la wanachama wa chama hicho waliofika makao makuu ya chama hicho usiku kujua hatma ya uongozi na viongozi wao.
Mbali na kumshukuru, alisema Profesa Lipumba ndiye mwasisi wa Ukawa na alikuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa Ukawa, kusisitiza kuwa alikaa na wenzake (wenyeviti wenza wa Ukawa) na kukubaliana kumkaribisha Lowassa ndani ya Ukawa.
"Na yeye ndiye aliyeanza kumsafisha mzee Lowassa. Nasema kwamba Ukawa ipo na imeimarika. Kwa kumuingiza Lowassa na nguvu za pamoja za vyama vinavyounda Ukawa ikiungwa mkono na wananchi wote wa Tanzania, Magufuli (John) hataiona Ikulu ya Kigamboni," alisema.
Wakati akitangaza kujivua uenyekiti, Profesa Lipumba alipoulizwa sababu za kugeuka wakati yeye alikuwa ni miongoni mwa wenyeviti wa Ukawa waliomkaribisha Lowassa, alikiri akisema kuwa suala la rushwa na ufisadi ni mfumo ambao lazima uondolewe lakini kwa sasa "dhamira yangu na nafsi yangu vinanisuta."
Katika maelezo yake ya juzi usiku, Maalim Seif alisema ana uhakika Ukawa itachukua dola kwa maelezo kuwa haitarudi nyuma na si dhamira yake kurudi nyuma.
"Lowassa ana msamiati wake kuwa kushindwa kwake mwiko, lengo letu ni moja tu, vyovyote itakavyokuwa tushike hatamu ya dola," alisisitiza Maalim Seif.
Kikao cha Dharura
Wakati hali ya sintofahamu ikiwakumba makada wa chama hicho, uongozi wa CUF umeitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi ili kutafuta mwanachama atakayekaimu nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Lipumba kitakachofanyika kesho.
Tamko hilo limetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa Ladhu, na kuwahahakikishia wanachama, wapenzi wa CUF na wananchi wa Tanzania kwamba chama hicho hakitayumba.
Alisema katika historia yake, CUF imepita katika dhoruba na misukosuko mingi, lakini mara zote imeonyesha uwezo mkubwa wa kuhimili na kukabiliana na athari zake.