Pichani ni muonekano wa Banda la Shirika la Umoja wa Mataifa Tanzania ndani ya Karume Hall katika maonyesho ya 39 ya kimataifa ya biashara 'Sabasaba', ndani ya viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, barabara ya Kilwa, jijini Dar. Pichani ni wananchi wakitembelea banda hilo na kupata taarifa mbalimbali za shughuli za Umoja huo nchini Tanzania.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu akitoa maelezo kwa mwananchi katika picha za viongozi mbalimbali waliowahi kuwa Makatibu wakuu wa Shirika la Umoja Mtaifa duniani ambalo hivi sasa linaongozwa na Ban Ki-Moon.
Pichani juu na chini ni Ismael Mnikite (kushoto) kutoka kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) akitoa maelezo ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa nchini kwa wananchi waliotembelea banda la Umoja wa Mataifa katika maonyesho ya 39 ya kimataifa ya biashara 'Sabasaba', ndani ya viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, barabara ya Kilwa, jijini Dar.
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu (katikati) akifafanua jambo kwa mdau wa Umoja wa Mataifa, Shaweji Steven (kushoto) aliyetaka kujua zaidi kuhusiana na ushiriki wa Umoja wa Mataifa katika tatizo la ajira za vijana nchini. Kulia ni Emmanuel Johnson kutoka Shirika la Afya (WHO) nchini.
Ismael Mnikite (kulia) kutoka kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), akitoa darasa la Malengo ya Maendeleo ya Millenia (MDG's) yanayotekelezwa na nchi wananchama wa Umoja wa Mataifa ambapo Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi wananchama kwa mmoja wa wananchi aliyetembelea banda hilo lililopo Karume Hall katika maonyesho ya Sabsaba.
Emmanuel Johnson (kulia) kutoka Shirika la Afya duniani (WHO) nchini akitoa maelezo ya ripoti ya UNDAP kwa mdau wa Umoja wa Mataifa, Shaweji Steven alipotembelea banda la Shirika la Umoja wa Mataifa kwenye maonyesho ya Sabasaba lililopo Karume Hall.
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu (kushoto) na Salome Mwambinga (wa pili kulia) kutoka (IAEA) wakihudumia wananchi waliotembelea banda la Shirika la Umoja wa Mataifa kwenye maonyesho ya sabasaba yanayoendelea kutimu vumbi jijini Dar.
Wananchi wakisaini kitabu cha wageni kwenye banda la Shirika la Umoja wa Mataifa.
Wananchi wakijichukulia vipeperushi mbalimbali vyenye taarifa za shughuli mbalimbali za Umoja wa Mataifa.
Na Modewjiblog team
Mtaalam wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu, amesema tangu Umoja huo ulipotoa fursa kwa wananchi wanaotembelea maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara ya sabasaba kutoa maoni kuhushu utendaji wake hapa nchini mpaka sasa zaidi ya watu 600 wameshiriki kutoa maoni yao.
Amesema watu waliotoa maoni hapo wametumia njia tofauti ikiwemo mtandao, ujumbe mfupi wa maandishi (sms), njia ya mdomo na kwa kuandika katika fomu maalum zinazopatikana katika banda lao
Bi. Temu amewashukuru wote walioshiriki kutoa maoni yao na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano pia katika mambo mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo inayoratibiwa na Umoja wa Mataifa nchini.
Jinsi ya kuendelea kushiriki kutoa maoni kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), kwa kuandika neno UN au UMOJA WA MATAIFA ambapo kwa watumiaji wa mtandao wa Airtel watatuma ujumbe wao kwenda namba 15453, kwa watumiaji wa mtandao wa Tigo wanatuma kwenda 15055 au 15453 na kwa Vodacom ni namba 15055 bila makato yoyote kwenye simu yako.
Ambapo pia njia nyingine ya kuwasilisha maoni yako moja kwa moja ni kupitia mtandao wa (Online) kwa kubofya link hii http://gpl.cc/UN2