Thursday, July 16, 2015

WAJAWAZITO KUTOZWA FEDHA WAKATI WA KIJIFUNGUA-MVOMERO


WAJAWAZITO KUTOZWA FEDHA WAKATI WA KIJIFUNGUA-MVOMERO


Wanawake wa vijiji  vya Mkindo na Mvomero,  wamelalamikia hospitali ya serikali ya Chazi kwa madai ya kuwatoza wajawazito Sh. 30,000  wanapokwenda kujifungua na kupima watoto wao kliniki.


Wanawake hao wametoa malalamiko hayo   mbele ya Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Wananchi (CUF),  Saverina Mwijage, wakati akiwa katika ziara yake kwenye vijiji hivyo ya kuhamasisha wanawake kujitokeza kuwania uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mmoja wa wanawake kutoka kijiji cha Mkindo Zaida Said, alisema wamechoshwa na  gharama kubwa wanazotozwa wanapokwenda kujifungua katika hospitali hiyo.
Alisema baadhi yao wamejikuta wakilazimika kujifungulia nyumbani kwa kushindwa kumudu gharama hizo.
Veronica Joseph, Mkazi wa Kijiji cha Mvomero,  alisema kuna wenzao na watoto wao wamekufa kwa kushindwa kupelekwa hospitali hapo kwa kukosa fedha.
Aliomba serikali kuwachukulia hatua wanaotoza fedha huduma hizo ambazo zinatolewa bure na serikali ili kuokoa maisha ya wajawazito na watoto.
Akizungumza na wanawake hao kwenye mkutano wa hadhara, Mwaijage, alisema suluhisho la matatizo yao ni kuchagua viongozi waadilifu kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ,Fatuma Kalembo,   alisema CUF haipo tayari kuona rasilimali za wananchi zinanufaisha vigogo wachache wa serikali huku wajawazito na watoto wakitozwa gharama za matibabu.
CHANZO: NIPASHE