Monday, July 06, 2015

SHERIA YA USIMAMIZI MAPATO YA GESI, MAFUTA YAPITISHWA



SHERIA YA USIMAMIZI MAPATO YA GESI, MAFUTA YAPITISHWA

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema sheria ya usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi ya mwaka 2015, itatumika katika usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi yatokanayo na shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi na Zanzibar itatakiwa kutunga sheria yake.


 
Akiwasilisha muswada wa sheria ya usimamizi wa mapato ya mafuta na gesi ya mwaka 2015, alisema mapato hayo yatokanayo na shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi kwenye miradi ya pamoja katika maeneo maalum au vitalu vinavyoingiliana kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, kwa mujibu wa sheria inayosimamia shughuli za mafuta za uendeshaji wa mkondo wa juu, kati na chini.
 
Alisema sheria hiyo itawezesha kuanzisha mfuko wa mapato ya mafuta na gesi utakaojumuisha akaunti ya kupokea mapato na akaunti ya utunzaji mapato.
 
Waziri huyo alibainisha vyanzo vya mapato vya mfuko huo kuwa ni mrabaha, gawio kutokana na ushiriki wa serikali kwenye shughuli za mafuta na gesi, faida ya serikali itokanayo na uzalishaji wa mafuta na gesi, kodi ya mapato ya makampuni yanayofanya utafiti, uchimbaji na uendeshaji wa rasilimali hizo, na faida kutokana na uwekezaji wa fedha zilizoko kwenye mfuko.
 
Alisema watafungua akaunti mbili ambazo ni akaunti ya kupokea mapato, ambayo itapokea mapato yanayoingia kwenye mfuko wa pamoja na akaunti ya utunzaji mapato, ambayo itahifadhi fedha kwa ajili ya uwekezaji wa fedha na kuhakikisha ustahimilivu na utulivu wa kibajeti.
 
Alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT), itapewa mamlaka ya kuendesha Mfuko wa Mapato ya Mafuta na Gesi kwa kuzingatia mwongozo wa kiutendaji.
 
Nyingine ni kuanzisha Bodi ya ushauri ya uwekezaji wa kifedha kwa ajili ya kumshauri Waziri wa Fedha kuhusu mikakati ya kiuwekezaji ya fedha zitakazohifadhiwa kwenye akaunti ya utunzaji mapato ya mfuko.
 
Alisema mambo mengine muhimu ni kuweka utaratibu wa matumizi ya mapato ya mafuta na gesi ambayo hayatavuruga utulivu wa uchumi kwa kuweka masharti ya kibajeti, yatakayotoa mwongozo katika kutoa fedha kwenye mfuko.
 
Alisema fedha hizo zitakwenda kwenye mfuko mkuu wa serikali kwa ajili ya kugharamia bajeti ya Taifa, sehemu kubwa ya fedha zitaelekezwa katika miradi ya maendeleo ya kimkakati ambayo itazingatia vipaumbele vya mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano.
 
Simbachawene alisema akaunti ya utunzaji mapato ya mfuko, zitatumika kuweka amana, kulinda ustahimilivu na utulivu wa kibajeti na kuwekeza kwa ajili ya kizazi kilichopo na vizazi vijavyo.
 
Alisema Kampuni ya Mafuta ya Taifa (NOC), itaweka utaratibu wa uhakika wa upatikanaji wa fedha za kugharamia shughuli za uwekezaji wa kimkakati ili kuongeza ushiriki wa nchi kupitia NOC katika kuwekeza kwenye sekta ya mafuta na gesi.
 
Aidha, alisema muswada huo utaweka masharti kuhakikisha mapato ya mafuta na gesi ya kwenye mfuko hayatatumika katika kukopesha au kudhamini mikopo kwa serikali, taasisi za umma na sekta binafsi au mtu binafsi. Muswada huo ulipitishwa.