Thursday, July 16, 2015

MZEE MWINYI MGENI RASMI SWALA YA EID EL FITR



MZEE MWINYI MGENI RASMI SWALA YA EID EL FITR

Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi (pichani), anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika swala ya sikukuu ya Idd El Fitr, ambayo kwa Mkoa wa Dar es Salaam itafanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.


 
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata)  limesema swala hiyo kesho au keshokutwa kutegemea mwandamo wa mwezi.
 
Baraza hilo pia limesema viongozi wengine wa Serikali watakaohudhuria katika tukio hilo ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na mabalozi kutoka nchi mbalimbali.
 
Akitoa taarifa hiyo jana jijini Dar es Saalam Sheikh wa Bakwata wa mkoa huo, Sheikh Alhad Musa Salum, alisema ibada hiyo inatarajiwa kuanza saa 1:30 asubuhi na akisisitiza kuwa siku ya Idd ni siku ya furaha na ya kuwasaidia wenye mahitaji mbalimbali.
 
"Siku kama hii Zakatul Fitr (sadaka) inapaswa kutolewa  kabla ya swala ya Idd kuswaliwa kwa yatima, wajane, maskini pamoja na kuwatembelea wagonjwa katika mahospitali kwa lengo la kuwafariji na kuwapa mahitaji kama ya chakula, kwani siku ya Idd haipaswi watu wenye shida kuombaomba chakula," alisema.
 
Alisema Waislamu na Watanzania wote wanapaswa kuitumia siku hiyo kumuomba Mungu ili Taifa libaki na amani kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi kwani amani ya nchi ni jambo muhimu kwa Taifa.
 
"Tunashukuru chama tawala CCM kimemaliza mchakato wake salama wa kupata mgombea wa nafasi ya urais, hivyo tunapaswa kuwaombea vyama vya upinzani waweze kukamilisha taratibu zao za kwa amani pia," alisema.