IRAN na mataifa sita yenye nguvu duniani wamefikia makubaliano muhimu leo mjini Vienna , kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kuweza kuondolewa vikwazo ilivyoekewa na mataifa ya magharibi Makubaliano hayo yamekuja katika siku ya 18 za mbio katika mazungumzo kati ya Iran na kundi la mataifa matano lijulikanalo kama P5 +1, mataifa matano ambayo ni Marekani , Urussi , China , Uingereza, Ufaransa pamoja na Ujerumani , mjini Vienna.
"Makubaliano yamekamilika," mwanadiplomasia mmoja ameliambia shirika la habari la AFP katika mji mkuu wa Austria , Vienna , mahali ambapo mkutano wa mwisho wa mawaziri kati ya Iran na mataifa makubwa uliitishwa.
Makubaliano yanatarajiwa kuzuia kwa kiasi kikubwa mpango wa kinyuklia wa Iran na kuweka ukaguzi mkali wa Umoja wa mataifa ili kuwezesha kuzuia kabisa utengenezaji wa silaha za kinyuklia na kufanya kuwa rahisi kugundua hatua kama hizo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Umoja wa Mataifa utafanya ukaguzi katika vinu vya nyuklia vilivyosambaa katika taifa hilo la kiislamu pamoja na kambi za kijeshi zitakazotiliwa shaka.
Kwa upande wa vikwazo vya mataifa ya magharibi vinavyoikaba Iran katika uuzaji wa mafuta na uchumi wa nchi hiyo yenye wakaazi milioni 78 vitaondolewa kwa taratibu.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif ameyasifu makubaliano ya kinyuklia kuwa ni "suluhisho la kila upande kushinda".
Ameongeza kwamba makubaliano hayo yanafungua upeo mpya kwa ajili ya kukabiliana na matatizo magumu zaidi ya dunia. Wakati huo huo waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameyaeleza makubalino hayo ni kosa kubwa la kihistoria na kusema atafanya kila kinachowezekana kuzuwia nia ya Iran ya kujipatia silaha za kinyuklia.
"Iran itapata njia ya uhakika kuelekea kupata silaha za kinyuklia, amesema Netanyahu. Vikwazo vingi ambayo vimekusudiwa kuizuia Iran kujipatia silaha hizo vitaondolewa," Netanyahu amesema mwanzoni mwa mkutano na waziri wa mambo ya kigeni wa Uholanzi Bert Koenders mjini Jerusalem.
"Iran itajipatia fedha nyingi, mabilioni ya dola , ambazo zitaiwezesha kuendelea na mabavu yake na ugaidi katika eneo hili na duniani. Haya ni makosa mabaya kabisa bila kiasi," amesema Netanyahu.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry na waziri mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif wamekuwa muhimu katika kumaliza mzozo huu kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran Kwa upande wake Rais wa Iran Hassan Rouhani katika akaunti yake ya Twiter amesema kufikiwa kwa makubaliano haayo ni ishara njema kwa Iran kuwa haikuwa na nia mbaya katika mpango wake wa nyuklia.
Taarifa rasmi kutoka kwa rais huyo wa Iran pamoja na mwenzake wa Marekani zinatarajiwa kutolewa wakati wowote baada ya kufikiwa kwa makubaliano hay leo.