Wabunge wawili wa Viti Maalumu (Chadema) wamekihama chama hicho na kujiunga na na vyama vingine huku mmoja akikiponda chama hicho kuwa hakina dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi.
Wabunge hao ni Chiku Abwao aliyehamia ACT – Wazalendo na Leticia Nyerere aliyerejea CCM.
Akizungumza katika ofisi za ACT, Dar es Salaam jana, Abwao alisema Chadema haina dhamira ya dhati kupambana na ufisadi kama ilivyokuwa inajibainisha miaka 10 iliyopita huku Leticia akieleza kuwa amerudi nyumbani kwa sababu amegundua kuwa uamuzi aliokuwa amefanya kwenda upinzani haukuwa sahihi.
Abwao ambaye amewahi kuwa mbunge kupitia NCCR-Mageuzi, alisema baada ya kutafakari, ameamua kujiunga na ACT – Wazalendo kwa sababu ameona kwamba kina dhamira ya kutaka kutatua matatizo ya wananchi.
"Leo nimejiunga rasmi na ACT na ninatangaza rasmi kuwa nitagombea ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini. Ninajiamini kwa sababu nina uzoefu wa kutosha," alisema mbunge huyo baada ya kukabidhiwa katiba ya chama hicho, Azimio la Tabora na fomu ya kugombea ubunge.
Alisisitiza kuwa amesoma katiba ya ACT, amesoma azimio la Tabora na kuona chama hicho kina mwelekeo wa kuwakomboa Watanzania kutoka katika umaskini unaosababishwa na ufisadi uliokithiri serikalini.
"Ninakwenda kupambana na CCM na Chadema kwa sababu hatuendani katika misingi ya siasa zetu. Ninajiamini, nina uwezo na nina uzoefu wa kutosha kuwaongoza Watanzania hasa wakazi wa Iringa Mjini," alisema.
Leticia alisema anaweza kuitumikia CCM bila hata ya kuwa mbunge kwani mchango wake unatambulika na anaweza kuleta maendeleo ndani ya chama na kwa wananchi.
"Nimekuwa nikisononeka kutokana na kukaa Chadema na kuacha kukaa kwenye chama kilichonilea na kunisomesha hadi nje ya nchi, kwa hiyo sasa nasema nimerudi nyumbani," alisema.
Alidai kwamba alifanya ujinga kwenda Chadema bila kutafakari na wala hawezi kulaumu dhamira yake ya kurudi katika chama kilichomlea na kuahidi kukitumikia kwa kasi itakayoleta maendeleo chanya kama alivyokuwa akichangia katika bungeni na sehemu mbalimbali.