WIKI moja kabla ya kwisha kwa muda wa warudisha fomu kwa makada wa CCM waliojitokeza kuwania kupitishwa na chama hicho kuwania urais wa Tanzania, ni wanachama sita tu kati ya 39 ndio waliorudisha fomu mpaka sasa.
Kwa mujibu wa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea wa urais ndani ya CCM, mwisho wa kurudisha fomu ni Julai 2, mwaka huu ambapo kila aliyechukua fomu anatakiwa kuwa na wadhamini 450 kutoka mikoa 15 ambapo mitatu iwe ya Zanzibar.
Idadi ya wanachama waliojitokeza mwaka huu inaonekana kuwa ni kubwa, mara tatu zaidi ya waliojitokeza mwaka 2005 ambapo wagombea walikuwa 11, ingawa Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyeibuka kidedea na kutetea tena ushindi wake mwaka 2010.
Waliorudisha fomu ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Makongoro Nyerere (Mbunge wa Afrika Mashariki), Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira na Balozi Ally Karume.
Wengine waliojitokeza kuchukua fomu ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Pia wamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge waSengerema, William Ngeleja, Mkazi wa Musoma mkoani Mara, Boniface Ndengo na mkulima kutoka Kijiji cha Mjimtala Wilaya ya Kasulu, Kigoma, Idelphonce Bilohe na Balozi Augustino Mahiga.
Wengine ni Dk Hans Kitime, Dk Mwele Malecela, Mbunge wa Nzega Dk Hamis Kingwangala, Balozi Amina Salum Ally, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Mtumishi wa CCM, Amos Siyantemi, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Wakili Mwandamizi Godwin Mwapongo, Peter Nyalile, Leonce Mulenda, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro.
WanaCCM wengine wanaoutaka Urais ni Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Monica Mbega, Patrick Chokala, Joseph Chagama, Malick Malupu, Ritha Ngowi na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Amos Robert.