Wednesday, June 24, 2015

Wagombea urais ccm wahamishia kampeni bungeni



Wagombea urais ccm wahamishia kampeni bungeni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akizungumza na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba bungeni mjini Dodoma jana. 
Harakati za wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana zilihamia katika ukumbi wa Bunge ambapo kila mmoja wao alikuwa akitafuta mbinu za kusalimiana na wabunge.
Hata hivyo baadhi ya wagombea hao walikuwa wanatumia nafasi hiyo kuzunguka na kuwafuata wabunge kwenye viti vyao, kiasi cha kufanya kuwepo na kile Spika alichokita kama ni vurugu ndani ya Bunge.
Spika Anne Makinda alilalamika mara kadhaa kuwa wabunge walikuwa wakifanya vurugu ndani ya ukumbi na kuwataka watulie, kwani wengi walikuwa wanapishana kwenye viti vya wagombea akiwamo Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ambaye kiti chake kilipata wageni wengi pia.
"Waheshimiwa wabunge naombeni utulivu basi, mbona mnaleta vurugu kwa kutembea tembea humu ndani wakati kanuni hazisemi hivyo, nitawataja kwa majina sasa," alisema Makinda.
Karibu wagombea wote ambao ni wabunge, naibu mawaziri na mawaziri jana walikuwa bungeni isipokuwa wagombea watatu wa CCM ambao ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala na Mbunge wa Kisesa, Luhwaga Mpina ndiyo hawakuonekana.
Mapema mgombea urais, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ndiye aliyekuwa wa kwanza kuvunja mwiko baada ya kuhama katika kiti chake anachotumia kila siku na kumfuata mgombea mwenzake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na wawili hao walitumia muda mrefu wakizungumza pamoja.
Kutoka hapo, Mwigulu alianza kuzunguka kwa staili yake kwa kwenda kwa wabunge huku akiwa makini kwa kukwepa viti walivyokaa wagombea wenzake, ambao wakati wote nao walikuwa na wabunge karibu yao wakizungumza.
Wagombea wengine waliokaa pamoja kwa muda mrefu ndani ya ukumbi ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri Mkuu Mizengo Pinda baada ya Magufuli kumfuata Pinda katika kiti chake.
Mgombea mwingine ambaye jana alionekana kutotulia katika kiti chake alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya.
Profesa Mwandosya huwa hana tabia ya kuhama kiti chake na kuwafuata wabunge au mawaziri na badala yake hufuatwa alipo, lakini jana hali ilikuwa tofauti.
Profesa Mwandosya alisalimiana na watu wengi ndani na nje ya ukumbi wa Bunge, ambako alikutana na wabunge kadhaa wa Mkoa wa Mbeya akiwemo mgombea mwenzake ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe na waliteta kwa muda.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa wabunge wengi kufika kumsalimia anapokaa na haikuwa jambo geni jana, kwani ni kawaida yake awapo ukumbini mara nyingi hukosa nafasi ya kupumua kutokana na msururu wa wabunge.
Hata hivyo, katika kiti ambacho wabunge hukitumia kuzungumza naye, jana kilitumika zaidi na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Juma Sadifa ambaye alikaa kwa muda mrefu zaidi wakiteta na alionekana kama ameziba nafasi ya wengine.
Nje ya ukumbi wa Bunge, Dk Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe waliongoza kupata watu wengi waliokuwa wakiweka msururu kuwasalimia.
Idadi kama hiyo pia ilikuwa kwa Pinda, ambaye licha ya kuwa na ulinzi, lakini nje ya ukumbi jana alisalimiana na watu wengi tofauti na siku zote.
Hata hivyo Pinda tofauti na siku zote jana alikuwa na staili tofauti kwani kila aliyemhisi kuwa alitaka kumpa walau mkono, alimfuata yeye na kusalimiana jambo lililowapa wakati mgumu walinzi wake kumzuia.
Mgombea pekee ambaye alikuwa na staili ya kwake katika salamu alikuwa ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ambaye toka ndani hadi nje alisalimia na watu wachache kwa kushikana mikono huku akionekana kuwapungia mikono zaidi.