Thursday, April 09, 2015

Mkurugenzi apingana na wananchi


Mkurugenzi apingana na wananchi
Msitu 
 Siku chache baada ya wananchi wilayani Mbinga kupinga uvunaji wa Msitu wa Mbambi, Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, Hussein Ngaga amesema huo ni ukikwaji wa sheria.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wananchi hao walizuia mbao zisiondolewe katika msitu huo kwa madai kuwa uvunaji unaoendelea utaathiri upatikanaji wa maji ambayo chanzo chake ni msitu huo.
Ngaga alisema juzi kuwa uvunaji wa msitu huo unafanywa kwa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha baraza la madiwani.
"Wilaya ina misitu sita ambayo utaratibu unaeleza kuwa itavunwa iwapo kutakuwa na dharura au mahitaji muhimu. Hayo yote yamejitokeza ndiyo maana baraza lilipitisha uamuzi wa kuvuna msitu huu," alisema Ngaga.
Alisema msitu huo ni mali ya halmashauri na kwamba ulianzishwa tangu mwaka 1984 na wananchi waliokuwapo eneo hilo baada ya kulipwa stahiki zao.
"Tunavuta msitu huu kwa sababu tumekubaliana na tumejiridhisha kuwa ni wakati mwafaka kufanya hivyo," alisema.
Ngaga alifafanua kuwa mahitaji yaliyochangia kufikia huo ni upungufu wa madawati 12,000 katika shule za msingi, ujenzi wa madaraja sita yaliyopo Mbinga Mjini, Maguu, Mapera na Kipapa.
"Tunayo misitu mingine ambayo ni Tukuzi, Mbuji, Ndengu, Mahenge na Lubera ambayo tumewapa Wilaya ya Nyasa ili wavune. Nawaomba wananchi wawe wavumilivu na waache dhana ya kuwa jambo hili linafanywa pasipo kufuata utaratibu," alisema.
Ngaga alisema wananchi wanapaswa kutambua kuwa miradi mbalimbali yenye manufaa kwao inatekelezwa kwa kuunganisha nguvu za wananchi.
Awali, wananchi hao walisema uvunaji huo unafanywa bila kuzingatia mahitaji yao na kwamba hawajashirikishwa.
Walisema shughuli hiyo inaendeshwa kwa masilahi binafsi ya baadhi ya watendaji wa wilaya ya hiyo.