Thursday, April 09, 2015

Tanroads, Polisi nao wabanwe katika matukio ya ajali



Tanroads, Polisi nao wabanwe katika matukio ya ajali

Jana katika ukurasa wa kwanza wa gazeti hili kulikuwa na habari iliyosomeka 'Uchunguzi wabaini sababu za kutokoma kwa ajali za barabarani'.
Habari hiyo ya uchunguzi, ilijaribu kueleza dhana mpya, tofauti na utamaduni uliozoeleka kwamba madereva ndiyo chanzo pekee cha ajali za barabarani.
Ni utamaduni uliozoeleka kwamba inapotokea ajali, mtu pekee wa kushughulikiwa ni dereva kwa kufikishwa mahakamani. Kuthibitisha hilo sasa hivi Serikali imeongeza kanuni kuwabana, kwamba kila baada ya miaka mitatu, warudi shule ya udereva na wakitenda kosa wanafutiwa leseni.
Si dhamira yetu kuwatetea madereva wazembe, walevi na wanaoendesha kwa mwendo usiostahiki, lakini ajali iliyotokea mwezi uliopita eneo la Mafinga Changalawe mkoani iringa ambako basi la Majinjah Express liligongana na lori na kusababisha vifo vya watu 42 na wengine kujeruhiwa, imetupa uwanja mpana wa kutafakari kwamba madereva siyo chanzo pekee cha ajali. Chanzo cha ajali ya Mafinga Changalawe ni shimo lililochimbika katika barabara hiyo ya lami inayosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Ujenzi, mtandao wa barabara nchini una jumla ya kilomita 87,581. Kati ya hizo kilomita 35,000 ni barabara kuu na za mikoa zinazosimamiwa na Tanroads. Zilizobaki ni za wilaya na ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi. Ajali ya basi la Majinjah Express ilitokea kwenye barabara iliyo chini ya Tanroads na inatupa fundisho kuwa kama wahusika wangetimiza wajibu wao vifo hivyo vingeepukika.
Habari tunayoiandikia maoni haya ilimnukuu mkurugenzi mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Ahmed Kilima akisema ajali za barabarani zina mazingira makubwa matatu, makosa ya kibinadamu, ubovu wa miundombinu na ubovu wa magari.
Tunaungana na Kilima kwamba kuna baadhi ya maeneo ya barabara yamekuwa chanzo cha ajali, mfano mashimo barabarani, kona kali, wembamba na sehemu nyingine hakuna alama za barabarani.
Kilima pia anazungumzia ubovu wa magari kwamba ni eneo jingine linalosababisha ajali, lakini ukimsikia Mnadhimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Johanes Kahatano, anakiri udhaifu katika ukaguzi wa magari na leseni, hasa wa mabasi. Anasema hawana vifaa vya kukagulia magari, wanachofanya ni kukagua kwa macho.
Kuna baadhi ya makandarasi ambao wametimiza wajibu wao kwa kujenga barabara zenye ubora ambazo zimesaidia kuepuka ajali za kizembe, mfano mzuri ni barabara ya eneo la Mikumi hadi Mafinga na barabara ya Chalinze-Segera. Lakini zipo barabara nyingine ambazo ujenzi wake ni vyanzo vikuu vya kutokea ajali za mara kwa mara.
Rai yetu ni kwamba pale inapobainika kuwa chanzo cha ajali ni miundombinu, basi wahusika walioshiriki kuitengeneza nao wawajibike, haitakuwa haki dereva ndiye awe mnyonge pekee wa kila ajali inayotokea.
Lakini hili la magari kukaguliwa kwa macho Serikali nayo haina budi kuwajibika. Haina sababu kuweka sheria kali kuubana upande mmoja na kuacha upande mwingine ambao nao unahusika kusababisha ajali za barabarani. Sheria msumeno.