Saturday, April 04, 2015

Mke wa Sumaye kunyang'anywa mashamba.

[image]
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani, imewataja vigogo
wanaohodhi maeneo makubwa ya ardhi bila ya kuyaendeleza na kuwapa siku
90 kuhakikisha wanayaendeleza, kinyume chake yatachukuliwa na Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tatu
Suleiman, ilisema vigogo hao walinunua mashamba katika eneo hilo na
kisha kuyaacha kwa muda mrefu bila kuyaendeleza akiwamo mke wa Waziri
Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Mama Ester Sumaye ambaye anamiliki
mashamba mawili, moja likiwa na ukubwa ekari 145.5 likiwa na namba
6069 na 6070 na shamba la pili lenye ukubwa wa ekari 103. 25 likiwa na
namba 6071 na 6075, yote yakiwa Misufini, Kibaha vijijini.

Taarifa hiyo inawataja watu wengine maarufu ambao wameshindwa
kuyaendeleza mashamba hayo kuwa ni, Phillipo Marmo ambaye ni Balozi
wa Tanzania nchini Ujerumani anayemiliki shamba 6159-6164maeneo ya
Kikongo, Nicodemus Banduka ambaye ni mkuu wa mkoa mstaafu wa mikoa ya
Pwani, Iringa na Mtwara anaye miliki shamba namba 1707 eneo la Vikuge
ambalo alilipata mwaka 2,000 na Kipi Warioba aliyewahi kuteuliwa
kugombea Ubunge Jimbo la Kawe ambaye anamiliki eneo Mperamumbi lenye
ukubwa wa heka 4000.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa, watu wengi walichukua mashamba katika
eneo hilo kuanzia miaka ya 1986 na kushindwa kuyaendeleza na
kusababisha kuwa mapori hali iliyopelekea halmashauri hiyo kufuata
sheria na kanuni zinazohusiana na umiliki wa ardhi.

Kufuatia mashamba hayo kutelekezwa, halmashuri ya wilaya hiyo inapanga
kuwasilisha taarifa hiyo kwa wizara husika ili miliki zake zifutwe
endapo wahusika watashindwa kuyaendeleza kwa muda waliopewa.

Tatu, alisema mwaka jana waliwataka watu wote waliochukua mashamba
hayo kuyaendeleza baada ya kufanyiwa uhakiki na baadhi ya watu
walijitokeza kuyaendeleza, lakini watu zaidi ya 40 hawajitokeza.

"Kutokana na kukahidi kuyaendeleza mashamba hayo, tumeshapeleka majina
ya wamiliki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wizara
imetutaka tutoe tena siku 90 kama hawatatekeleza kwa kipindi hicho,
watajua nini cha kufanya,'' alisema.

Gazeti hili lilipowasiliana na Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye kwa njia
ya simu ili kuzungumzia taarifa za mkewe kushindwa kuyaendeleza
mashamba hayo kwa kipindi kirefu, alisema hana taarifa zozote za mkewe
kushindwa kuyaendeleza mashamba hayo anayomiliki.

''Wewe ndiyo nakusikia, sisi hatujaliona hilo tangazo, wala mke wangu
hana hizo taarifa ila baadaye tutakapoziona tutakupigia simu
tuwasiliane,'' alisema Sumaye.