Wednesday, March 25, 2015

Ngonyani: Siombi Radhi,Nipo Tayari Kwa Lolote....Nilienda Kwa LOWASSA Kwa Ridhaa Yangu na Sitaki Mtu Anichagulie Marafiki



Ngonyani: Siombi Radhi,Nipo Tayari Kwa Lolote....Nilienda Kwa LOWASSA Kwa Ridhaa Yangu na Sitaki Mtu Anichagulie Marafiki
MBUNGE wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani (CCM) ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Umoja wa Wazazi Taifa,   amesema wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, hapaswi kutafutiwa marafiki wala ndugu walioonesha dhamira ya kuwania uongozi ndani ya chama na kuwaunga mkono.

Alisema kitendo chake cha kwenda nyumbani kwa mwanachama wa CCM anayedaiwa kutaka kuwania nafasi ya urais kwenye Uchaguzi Mkuu, kisitafsiriwe vibaya au kuchafuliwa kisiasa.

Bw. Ngonyani aliyasema hayo mjini Dodoma jana siku moja baada ya Jumuiya ya Wazazi Taifa, kutoa mwezi mmoja kwa baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wazazi akiwemo mbunge huyo kuomba radhi kwa kutumia jina la jumuiya hiyo vibaya.

Jumuiya hiyo inadai baadhi ya wajumbe hao ni miongoni mwa makundi ya watu waliokwenda nyumbani kwa mwanachama wa CCM, kumshawishi achukue fomu ya kuwania urais na kumchangia fedha wakitumia jina la jumuiya.

Tamko la jumuiya hiyo lilitolewa na Mwenyekiti wake, Bw. Abdallah Bulembo, akimtaja Bw. Ngonyani kuwa miongoni mwa wajumbe wa baraza wanaopaswa kuomba radhi bila kumtaja mwanasiasa aliyetembelewa akisema ni mtu anayefahamika na wengi.

Akijibu tuhuma hizo, Bw. Ngonyani alisema yupo tayari kwa lolote; lakini hawezi kuomba radhi kwani yeye pamoja na wenzake walikwenda nyumbani kwa Mbunge huyo wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa; si kwa kutumia nembo ya jumuiya hiyo.

"Hatukwenda nyumbani kwa Lowassa kuomba fedha au chakula; bali tulikwenda kwa mapenzi mema...mimi kama ilivyo kwa wajumbe wengine, nilipata taarifa za kwenda kumsalimia Bw. Lowassa nyumbani kwake.

"Kwa sababu ya ukaribu wangu na Lowassa, sikusita kwenda lakini si kwa kuwakilisha nembo ya jumuiya hiyo na wala hatukuhongwa kufanya hivyo," alisema Bw. Ngonyani.

Alisema yeye kama mbunge, atamshabikia mtu ambaye yupo ndani ya roho yake na kuongeza kuwa, ataendelea kwenda kwa Bw. Lowassa hadi kieleweke na kama kuna
hatua za kuchukuliwa dhidi yake yupo tayari na huyo anayesema wao wana makosa naye ajichunguze.

"Nashangaa kusikia mimi ndiye niliyetoa fedha na kuwapa wajumbe wenzangu tuliokwenda nyumbani kwa Lowassa jambo ambalo linanisikitisha sana kwa mtu maskini kama mimi kutafuta watu niwape fedha ili waende kwa Lowassa.

"Tulienda kwa mapenzi yetu kupitia umoja ambao tulikuwa tumekubaliana, nipo tayari kukosa ubunge, naweza kurudi katika fani yangu ya uganga, kabla sijawa mbunge nilikuwa huko; lakini viongozi mbalimbali walinishawishi nigombee ubunge na kuipata nafasi hiyo," alisema.

Mjumbe mwingine wa baraza hilo mkoani Njombe, Evarist Lupenda, alisema yeye ni miongoni mwa watu waliokwenda nyumbani kwa Lowassa kwa matakwa yake si kushawishiwa.

Alisema yeye na wenzake walipewa taarifa ya kwenda kwa Lowassa kumsalimia na hawakutumia jina la jumuiya hiyo na matamko yaliyotolewa hayakuwa ya jumuiya.

Aliongeza kuwa, kama imefikia hatua ya kutishana wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, viongozi wengi ambao tayari wameonesha kuwa karibu na Lowassa akiwemo Mwenyekiti  wa CCM mkoani Shinyanga, Hamis Mgeja, Mgana Msindai wa Singida, basi chama kiwachukulie hatua na hao.

"Bulembo lazima azifanyie uchunguzi taarifa anazopelekewa kabla ya kutoa matamko," alisema.

Naye mjumbe wa baraza hilo mkoani Dodoma, Mchungaji Damas Mkasa, alisema sh. 600,000 walizomkabidhi Bw. Lowassa ili kumshawishi achukue fomu walijichangisha wenyewe sh. 20,000 kila mmoja na hazikutolewa na Bw. Ngonyani.