Imeelezwa kuwa imani za kishirikina ndiyo chanzo cha walimu kushindwa kufundisha maeneo ya vijijini pindi wanapopangiwa kutokana na kutishiwa maisha wanapotoa adhabu kwa wanafunzi wao.
Mratibu Elimu Kata ya Mvomero, Malonga Dilukwili alisema hayo jana alipozungumza na walimu, maofisa watendaji wa vijiji na madiwani kwenye mafunzo ya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha katika elimu yaliyoandaliwa na Asasi ya Elimu na Mazingira (Wetu) mkoani hapa.
Dilukwili alisema maeneo mengi ya vijijini yamekuwa na sifa zinazoogopesha wageni wanaofika katika maeneo yao kwa kuendekeza ushirikina.
"Inasikitisha, walimu wamekuwa wakijitolea kufundisha lakini wenyeji wanawatolea maneno ya vitisho kuwa wataondoka. Sasa kwa mtindo huu elimu itapanda maeneo ya vijijini?" alihoji Dilukwili.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dk Joseph Saqware alisema ili elimu ikue maeneo ya vijijini, ni lazima wazazi na walimu washirikiane katika kukuza sekta hiyo. Alisema licha ya walimu kuogopa, lakini miundombinu ya shule za vijijini haikidhi vigezo vya kufundishia wanafunzi.
Aliiomba Serikali kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya shule hizo, huku akisisitiza wazazi na walezi kuacha kuwatolea walimu lugha za kutisha.