Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.
Matukio ya kuvamia, kupora silaha na kuua askari katika vituo vya polisi yameelezwa na Jeshi la Polisi kuwa huenda wahalifu wanafundishwa na makundi ya kigaidi yanayofanya uhalifu katika baadhi ya nchi za Afrika kama vile kundi la Boko Haram.
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, akizungumza katika mahojiano maalum jana jijini Dar es Salaam, alisema kila siku jeshi hilo limekuwa likijitahidi kupambana na mauaji, wizi na ujambazi, lakini bado matukio hayo yanaendelea kutokea nchini.
IGP Mangu alisema kinachofanywa hivi sasa na Jeshi la Polisi ni kubadilisha mbinu za kiulinzi na kuachana na za kizamani kwa sababu jeshi hilo halikuwahi kufikiria kama kuna siku vituo vya polisi vitavamiwa kama inavyotokea sasa na hivyo imekuwa ni changamoto kubwa na mpya kwa jeshi hilo.
"Uhalifu ni kama upepo ukitokea kwa jirani hapo hakuna namna ya kuzuia huo upepo usijekutupuliza na sisi, cha msingi baada kupulizwa mnashtuka namna gani mtapambana nao kama mtaweza kubadilika mbinu au mtaendelea kubakia katika utendaji kazi wenu na mambo ya zamani," alisema.
Alisema suala la kwamba majambazi wamekuwa na nguvu kuzidi jeshi hilo na ndiyo maana matukio haya yanatokea siyo la kweli, kwa sababu dunia sasa inabadilika na matukio ya kupora silaha na kuua askari yamekuwa yakitokea hata katika nchi jirani kama Kenya.
"Haya matukio yanatokea hata kwa jirani zetu kama Kenya, askari wananyang'anywa silaha, kundi kama la Boko Haram wanavamia vituo vya polisi na kupora silaha, kwa hiyo lazima tutambue kuwa Tanzania siyo kisiwa, hao wahalifu waliopo huko inawezekana wakawa wanafundisha na hawa kwetu kufanya uhalifu hapa nchini," alisema.
Alisema jambo la msingi ni kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahalifu ili hatua zichukuliwe dhidi yao na Tanzania iendelee kuwa nchi ya amani.
Katika kipindi cha kuanzia Januari mwaka huu kumetokea matukio mfululizo ya uvamizi wa vituo vya polisi ambavyo vinaporwa silaha, kuua na kujeruhi askari, hali ambayo imeleta hofu kwa wananchi kuhusu hatma ya usalama wao hasa katika kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu.
Tukio kubwa lililotikisa ni lile lililotokea mwezi uliopita baada ya watu 10, wanadhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za jadi na za moto walipokiteka kituo cha polisi Ikwiriri kilichopo tarafa ya Ikwiriri, wilayani Rufiji, mkoani Pwani na kuwaua askari wawili, kupora silaha saba na kisha kulipua bomu kituoni hapo.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Pwani, Urich Matei, aliwataja askari waliouawa katika tukio hilo kuwa ni PC Judith Timoth na Koplo Edgar Mlinga.
Alisema katika tukio hilo majambazi hao ambao hadi sasa hawajakamatwa wala silaha walizopora hazijapatikana, baada ya kukivamia kituo hicho walifanikiwa kuiba silaha aina ya SMG (Sub Machine Gun) mbili, SAR mbili, Shortgun moja na bunduki mbili za kulipulia mabomu ya machozi.
Siku chache baada ya tukio hilo, watu wengine wanaosadikiwa kuwa majambazi waliwavamia askari polisi wawili waliokuwa doria Mjini Tanga na kuwapora bunduki mbili aina ya SMG kisha kumjeruhi kwa kumchona kisu mmoja wao.
UVAMIZI MGETA
Tukio lingine ni la mkoani Morogoro, Wilaya ya Kilombero, ambako watu wanaodhaniwa kuwa majambazi walivamia kituo kidogo cha polisi Mgeta na kupora SMG moja na magazine moja yenye risasi 30.
Katika tukio hilo, wavamizi hao walipora vitu mbalimbali ambavyo ni vielelezo vya ushahidi kwenye kesi inayomkabili mtuhumiwa Emmanuel Shewele (21).
UVAMIZI MKAMBA
Matukio mengine yalitokea Juni 11, mwaka jana baada ya watu wasiojulikana walipokivamia kituo kidogo cha polisi Mkamba mkoani Pwani na kusababisha kifo cha askari mmoja na mgambo.
Askari aliyefariki ni mwenye namba D 9889 koplo Joseph Ngonyani ambaye alifia katika hospitali ya wilaya ya Mkuranga wakati akitibiwa kutokana na kumkatakata na mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
Katika tukio hilo, askari mgambo Venance Francis naye alifariki wakati akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) huku askari Mariamu Mkamba aliyejeruhiwa akipatiwa matibabu na kupona.
Majambazi hayo katika tukio hilo walipora silaha aina ya Shortugun tatu, Sub Mashine Gun (SMG) mbili na magazine 30 kila moja ambazo zilikuwa kwenye ghala la muda zikisubili kupelekwa kwenye kituo kikubwa penye ghala kuu la silaha.
UVAMIZI USHIROMBO
Tukio jingine la kuvamiwa kituo cha polisi lilitokea Septemba mwaka jana katika kituo kikuu cha polisi wilayani Bukombe mkoani Geita ambako askari wawili waliuawa na kujeruhi wengine watatu. na bunduki 10 kuporwa.
Mbali na kupora SMG 10, pia inadaiwa walifanikiwa kupora risasi ambazo idadi yake haikutambulika mara moja pamoja na mabomu ya kutupa kwa mkono na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Joseph Konyo aliwataja askari waliouawa kuwa ni WP 7106 Uria Mwandiga na G. 2615 PC Dustani Kimati na waliojeruhiwa askari namba E.5831 CPL David Ngupama Mwalugelwa aliyejeruhiwa kichwa na usoni huku akiumizwa mdomo na meno mawili kungooka pamoja na Mohamed Hassan Kilomo amabye alijeruhiwa kifuani na mguu wa kulia kwa risasi.