KUSHUKA kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hakujawapa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) unafuu wa kuwafanya washushe bei ya umeme.
Aidha, serikali imesema haifumbii macho suala hilo na imeziagiza Mamlaka husika za Tanesco na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), kuangalia inapotokea fursa, ili iweze kwenda kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Igalula, Athumani Mfutakamba (CCM), aliyetaka kufahamu sababu za kushuka kwa bei ya mafuta duniani.
Alihoji, kutokana na anguko hilo kwa nini gharama mbalimbali, ikiwemo bei ya umeme unaozalishwa na TANESCO, IPTL, Aggreko, Symbion haujashuka wakati mafuta yameshuka bei.
Akijibu swali hilo, Mwijage alisema uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini kwa sasa ni MW 1,226.24 ,mitambo ya kufua umeme kwa maji inazalisha MW 561.84, gesi MW441, na mafuta MW 223.40.
Alisema kampuni za IPTL na Aggreko zinaiuzia Tanesco umeme kwa senti za Marekani 28 hadi 40 kwa uniti wakati Tanesco inawauzia wananchi umeme kwa senti za Marekani 16.4 kwa uniti.
"Kwa kuangalia takwimu hizo, ni dhahiri kuwa Tanesco inanunua umeme kwa bei juu kuliko inavyowauzia wananchi, hivyo kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hakujawapa nafuu wa kufanya washushe bei," alisema Mwijage.
Alisema hali ya kushuka kwa bei za nishati ya mafuta duniani imetokana na kudorora kwa uchumi katika bara la ulaya, kuongezeka kwa matumizi ya nishati mbadala, kuimarika kwa utumiaji mzuri wa mafuta na ufanisi wa tija katika kuzalisha mafuta kutoka miamba ya Shale na mengineyo.