Thursday, February 05, 2015

WAJAWAZITO WAJIFUNGUA KWA KIBATARI





Kituo cha Afya cha Msanda Muungano kilichopo wilayani Sumbawanga Mkoa wa Rukwa, kinalazimika kutumia chumba kidogo, mwanga wa kibatari na mshumaa nyakati za usiku kwa ajili ya wajawazito kujifungua.

Kutokana na hali hiyo, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Charles Apolinary ameishauri Serikali kukishusha hadhi kwa kutokidhi mahitaji.
Dk Apolinary alisema hayo juzi alipozungumza na viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania CCM (UWT) Wilaya ya Sumbawanga waliotembelea kituoni hapo katika kusherehekea miaka 38 ya chama hicho.
Alisema kituo hicho kina ukosefu wa nishati ya umeme hali inayoleta usumbufu wakati wa kutoa huduma za afya.
Dk Apolinary alisema ukosefu wa dawa kwa miezi kadhaa pia umekuwa kero kwa wagonjwa ambao huenda kituoni hapo kwa ajili ya kupima, lakini dawa hununua katika maduka binafsi.
"Ni aibu kituo hakina hata dawa za kutuliza maumivu na bado unaita ni kituo cha afya? Kwa nini wasikishushe hadhi kiwe zahanati, kwa kuwa kuna zahanati nyingine dawa zipo.
"Hapa changamoto ni nyingi, kuna tatizo la upungufu wa nyumba za watumishi, zilizopo ni mbili," alisema Dk Apolinary.
Alisema wajawazito wanaotakiwa kujifungua kwa upasuaji hupewa rufaa kutokana na kituo hicho kutotoa huduma hiyo.
Mwenyekiti wa UWT, Sumbawanga, Scolastica Malocha alisikitishwa na ukosefu wa vifaa tiba na dawa katika kituo hicho.
Hata hivyo, alisema ataziwasilisha taarifa hizo kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ili kuhakikisha kituo hicho kinafanya kazi kwa hadhi yake.
"Nimeona kuna haja ya kuongeza majengo, hata haya yaliyopo yalijengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) awamu ya kwanza na hayatoshi.