Serikali imetakiwa kukamilisha haraka mchakato wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu ili kuwafanya walimu waipende kazi yao na kuendelea kufanya kazi maeneo ya pembezoni.
Mwenyekiti wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Magreth Sitta, alitoa wito huo jana wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati yake bungeni jana.
Alisema idadi kubwa ya walimu wanaoteuliwa kwenda kufundisha katika maeneo ya pembezoni ama hawaendi kabisa au wanapokwenda hawaka kwa muda mrefu kutokana na mazingira hayo kutokuwa rafiki.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo umefika wakati ambao sasa Serikali ikamilishe mchakato wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa walimu hao ikiwa kama motisha wa kuwafanya wasiondoke kwenye mazingira yao ya kazi.
"Ili kuimarisha utoaji wa elimu hususan katika maeneo ya pembezoni, Serikali ikamilishe mapema iwezekanavyo mchakato wa kutoa posho ya mazingira magumu kwa walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu ili kuwafanya wabaki kazingira ya kazi ikiwamo kuipenda kazi yao," alisema Sitta.
Aidha, aliitaka Serikali kuweka mkakati wa makusudi wa kuboresha mazingira ya utoaji elimu kwa watu wenye mahitaji maalum kwa kutenga fedha za kutosha kwenye sekta hiyo.
Sitta alisema kuwa katika mkakati huo, Serikali pia itoe mwongozo wa kitaifa kuhusu ujenzi wa miundombinu ya shule na vyuo na kutaka usajili wa shule na vyuo hivyo uzingatie mahitaji ya kundi la watu wenye mahitaji maalum.
Katika mapendekezo ya Kamati yake, Sitta pia aliitaka Serikali kukabiliana na ongezeko la vyuo vinavyotoa elimu ya ufundi bila kuzingatia vigezo vilivyowekwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte).