Wednesday, February 04, 2015

Spika Makinda aunga mkono ‘mwendo wa kinyonga’ wa serikali kuhamia Dodoma



Spika Makinda aunga mkono 'mwendo wa kinyonga' wa serikali kuhamia Dodoma
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda(pichani), ameunga mkono 'mwendo wa kinyonga' unaofanywa na Serikali kuhamishia makao Makuu ya nchini mkoani Dodoma.
 
Alitoa kauli hiyo bungeni jana baada ya Naibu wa Wizara ya  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agrey Mwanri  kujibu swali la Mbunge wa Chilonwa (CCM), Hezekia Chibulunje kutaka kujua sababu za mswada wa kutambua Dodoma kuwa makao makuu ya nchi kuchelewa kuwasilishwa bungeni.
 
Mwanri alisema  utekelezaji wa sheria ya kutambua Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, ikiwamo ukomo wa muda ambao Serikali itahamia utawekwa kwa utaratibu mahsusi, kupitia kanuni  zitakazotungwa na Waziri mwenye dhamana ya Ustawishaji Makao Makuu.
 
Alisema kwa sasa  Waraka wa Baraza la Mawaziri wa kutunga Sheria hiyo, uko katika hatua ya kupata maoni ya sekretarieti yake  hivyo bado kuna hatua mbili katika mfumo wa kuandaa muswada  huo kabla ya kuwasilishwa bungeni.