Friday, February 06, 2015

Mtanzania wa kwanza mwenye leseni ya uhakiki ndege kimataifa


Mtanzania wa kwanza mwenye leseni ya uhakiki ndege kimataifa
Leseni ni kibali maalumu kwa kazi maalumu, biashara au huduma anayopewa mtu au kikundi kwa lengo la kutekeleza shughuli zake kihalali baada ya kutimiza sifa au matakwa yaliyowekwa.
Hivyo ndivyo ilivyo kwa Stanslaus Maganga, ana leseni ya kimataifa ya kuongoza ndege. Si kusimama mbele ya ndege na kuiongoza, wakati wa kutua, la hasha.

Leseni aliyonayo ni ya kudhibiti ubora na uimara wa ndege. Ndege yoyote haiwezi kurushwa bila saini ya Mhakiki Ubora (Quality Assurance Inspector), ambaye ni Maganga.
Anahakikisha injini iko sawa, kiasi cha mafuta kinawiana na umbali, uwiano wa abiria na mizigo na ndipo anasaini kuruhusu ndege kupaa.
Katika mahojiano maalumu, Maganga aliyezaliwa Desemba 14, 1983 anasema kumekuwa na malalamimiko ya abiria kuchelewa au kuvunjwa kwa safari, hilo kwa upande wake haliwahusu.
"Kitengo changu huwa tunagombana sana na utawala au watu wa masoko, lakini tunachoangalia ni usalama wa abiria kwanza.
"Wao wanatukabidhi ndege, kuiangalia ikijiandaa kwa safari, sasa tunahakikisha iko kwenye ubora wa kuruka kwa asilimia 100, hata muda ukifika, kama ndege haijatengemaa, hatuwezi kuwakakabidhi.
"Ndiyo maana utasikia, ndege imeahirisha safari, ndege imefuta safari zake, hiyo yote ni kutokana na kwamba bado iko kwenye matengenezo.
"Hata abiria wakilalamika, walie machozi, hatuwasikilizi kwa sababu uimara wa ndege, ubora wa ndege ni kwa usalama wao, sasa unakabidhi ndege eti kwa sababu tu muda umefika, unaweza kusababisha madhara," anasema Maganga ambaye ndiye fundi mkuu wa Shirika la Ndege la Precision.
Alivyoipata nafasi
Anasema, baada ya kumaliza Chuo cha Ufundi na Teknolojia, DIT, Dar es Salaam 2003, aliingia mtaani. "Nilifanya kazi za kubangaiza, lakini baadaye nikapata kazi katika kampuni ya Simu ya Zantel kufunga mitambo yake.
"Nikiwa Zantel tulifunga minara yao maeneo mengi, kuanzia Dar es Salaam, Bagamoyo, Gairo na Dodoma.
"Pia tulifunga mitambo katika mikoa ya Kusini, Rufiji, Nangulukulu hadi Mtwara, nilikuwa fundi kiongozi…sijui waliniamini nini, lakini nilikuwa kiongozi," anasema.
Anasema hata hivyo aliachana na Zantel na kujiunga na Kampuni ya simu ya Hits.
"Nikiwa kazini Hits, nilinunua Gazeti Mwananchi na kuona tangazo la Kampuni ya Precision kwamba inatoa scholarship za kusomea ufundi wa ndege.
"Niliomba na bahati nzuri nikakubaliwa. Tulikuwa wanne na tulipelekwa kwenye mji wa Toulouse, Ufaransa kwenda kusomea kazi hiyo.
"Sasa, ni kama ajabu. Hili la ndege lilikuwa kichwani mwangu siku nyingi. Nilipokuwa mdogo nilikuwa najiuliza sana, hivi ndege kwanini inapaa, kwanini haianguki wakati ni nzito, watu wanakaa kaaje ndani?
"Hii ilikuwa ikinijia sana kwa kuwa nilikuwa nasoma Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, Dodoma ninapoona ndege inatua au kuruka. Nikasema siku moja na mimi nataka niendeshe ndege."
Anasema walipofika Ufaransa, walikutana na mambo mengi mageni, lakini walikabiliana nayo.
"Tulifundishwa ufundi wa ndege na tulikuwa tunafanya kazi na mashirika makubwa, Air France na tulikwenda wanakotengeneza ndege za aina mbalimbali.
"Tulikwenda wanakotengeneza boeing, wanakotengeneza ndege aina ya Airbus, ATR, ndege zote za vita air force na wanakorusha ndege za masafa ya mbali wanaziita air space…zaidi tulikuwa tunasomea kwa vitendo jinsi ya kutengeneza injini na mfumo mzima na umeme katika ndege.
"Tumesomea zaidi utengenezaji wa ndege aina ya boeing na zaidi ni mfumo wa injini na maeneo mengine mengi ya ndege," anasema.
Anasema akiwa Toulouse, alikumbana na changamoto mbalimbali kwani Ufaransa wamepiga hatua za mbali kwa teknolojia ikilinganisha na Tanzania, lakini taratibu walizoea.
Anasema Watanzania walio wengi wanakosa nidhamu ya muda.
"Kule wako makini sana na muda, hakuna muda unaopotea kizembezembe, hakuna ubabaishaji, na suala la ndege ni umakini asilimia 100, hivyo hakuna kubabaisha," anasema.
"Baada ya mwaka mmoja darasani, tangu 2009 tulifanya mafunzo kwa vitendo kwa miaka mitano hadi 2013, pamoja na mfunzo mengi ya mara kwa mara na hadi leo hii nina leseni ya kimataifa, inaitwa EASA 66.
"Hii leseni European Aviation Safety Agency 66, inaniruhusu kufanya kazi popote Ulaya na Amerika kwani pia nina leseni ya FAA inayotambulika Marekani, nina uwezo wa kuruhusu ama kuikataa ndege kuruka popote duniani," anasema.
Kazi baada ya mafunzo
Anasema baada ya kurudi nyumbani, waliendelea na kazi PrecisionAir na zaidi ni kitengo cha ubora. "Unajua ndege haiwezi kuruka bila watu kama mimi, kwa nafasi hii tuko wachache nchini.
"Mashirika mengi ya ndege yameajiri watu kutoka nje… wanatoka Malawi, Zambia, Afrika Kusini na hata Ulaya kwa kuwa hakuna Mtanzania mwenye sifa kufanya ukaguzi wa ndege… ninashukuru nimefikia hatua hii," anasema.
Mipango yake
Anasema baada ya mafunzo na kupata leseni hiyo, anatamani kuona Watanzania wengi wanaingia kwenye kazi kama yake, ambayo anasisitiza kuwa inahitaji uvumilivu.
Maganga ambaye ameoa na ana mtoto mmoja, anasema kwa sasa anachokifanya ni kutoa mafunzo kwa mafundi wanaochukua mafunzo hayo ngazi za chini... "Ninatamani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wangekuwa na shahada ya uhandisi wa ndege, angalau tungekuwa na watu wetu," anasema.
Anasema wapo wanaokuja kufanya kazi kwa vitendo ambao anaamini wakiendelezwa, watakuwa na nafasi nzuri.
Maganga anasema pia kuwa, kufanya kazi kama anayoifanya, kunahitaji uvumilivu wa hali ya juu, nidhamu pamoja na kutuliza akili.
"Ukipewa jukumu kama langu, kwa yeyote, inatakiwa kutuliza akili. Huwezi kufanyafanya tu kukimbizana na muda ukabidhi kazi, hapana. Hapa nidhamu ya kazi ndicho kitu cha kwanza.
"Vilevile, nidhamu katika chakula. Kazi ya injinia wa ndege hutumia akili nyingi na nguvu kiasi fulani, sasa kuna vyakula maalumu vya kuchangamsha ubongo na mwili.
"Tulipokuwa Ufaransa, tulikuwa tunakula zaidi chokoleti na matunda aina ya kiwi, hivi vitu vinajenga sana akili… nidhamu ya chakula ni muhimu," anasema.
Mkurugenzi amsifu
Mkurugenzi Mkuu wa Precision, Sauda Rajab anasema mpango wa shirika ni kusomesha vijana wengi zaidi wa Tanzania kuliko kutegemea wataamu wa kigeni.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kumkabidhi leseni yake, alisema mafunzo kama hayo ni gharama kwani mtu mmoja husomeshwa kwa Euro 75,000 (Sh148 milioni).
Anampongeza Maganga na kusema kuwa mpango pia ni kutoa huduma zaidi kwa mashirika mengine ya ndege.