Kuna taarifa za kusikitisha juu ya kutekwa kwa mtoto mwingine mwenye ulemavu wa ngozi (albino) usiku wa kuamkia juzi katika Kijiji cha Ilelema, wilaya ya Chato mkoani Geita.
Ilielezwa na jeshi la polisi mkoani humo kuwa wavamizi walifanikisha nia ya ovu baada ya kumvamia mama wa mtoto aliyekuwa jikoni akipika majira ya saa 2:00 usiku, wakamcharanga mapanga na baadaye ndipo wakamteka mtoto huyo aitwaye Yohana Bahati, mwenye umri wa mwaka mmoja.
Mama wa mtoto huyo, Esther Bahati, aliyekuwa amepambana kadri ya uwezo wake kuzuia mwanawe asitekwe, alikimbiziwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita na baadaye akahamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya usoni, mikononi na mabegani.
Hakika, taarifa hizi zinasikitisha. Ni muendelezo wa vitendo vya kinyama dhidi ya albino, hasa katika mikoa ya kanda ya ziwa kama Mwanza na Geita. Sisi tunalaani vikali kitendo hiki.
Ni imani yetu kwamba jeshi la polisi, kwa kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Ilelema na kwingineko nchini watafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba mtoto huyo anapatikana.
Tukio hili la juzi limejiri ikiwa ni siku takriban 50 tu tangu mtoto mwingine albino aitwaye Pendo, mwenye umri wa miaka minne, kutekwa kutoka mikononi mwa wazazi wake wakati wakiwa nyumbani kwao katika Kijijini cha Ndami, Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza. Na hadi sasa mtoto huyo pia hajapatikana.
Tunatambua kwamba kufikia sasa, zipo jitihada kadhaa zimechukuliwa katika kuwabaini wahusika wa uhalifu huo. Hata hivyo, kasi hii mpya ya kutekwa watoto albino inadhihirisha kwamba mikakati ya kuwanasa watendao unyama huu bado haijafanikiwa.
Kwa mfano, takwimu zilizowahi kutolewa jijini Dar es Salaam mwaka jana na Chama cha Albino Tanzania (TAS), wakati wa maadhimisho ya Siku ya Amani ya Kimataifa ya Albino inayoadhimishwa Septemba ya kila mwaka, zilionyesha kuwa kutoka mwaka 2006, albino 74 walishauawa kikatili, huku 56 wakinusurika kifo na kati yao, albino 11 waliongezewa ulemavu mwingine wa kudumu.
Ilielezwa zaidi kuwa hadi kufikia Septemba mwaka jana, kulikuwa na matukio zaidi ya 100 yanayohusisha vitendo vya ukatili dhidi ya albino lakini kati yake, ni 11 tu ndiyo yaliyofikishwa mahakamani na kesi tano kati ya hizo ndizo zilizotolewa hukumu.
Sisi tunaamini njia mojawapo ya kufanikiwa vita hii ni kuhakikisha kwamba vitendo vinatangulizwa zaidi katika kukabiliana na wahalifu hawa badala ya mfululizo wa matamko makali na viapo vya midomoni.
Kwa mfano, tunadhani kwamba utekelezaji wa kila kilichoelezwa bungeni mwaka 2009 na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumzia ukatili huu unaolitia aibu taifa ni njia mojawapo ya kukomesha vitendo hivi.
Kama hiyo haitoshi, operesheni iliyotangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani hivi karibuni katika kuwabaini na kuwatia mbaroni waganga wa jadi wanaotumia ramli inapaswa kuzaa matunda kwa kutekelezwa kivitendo, kwani imethibitika pasi na shaka kuwa watu hawa (waganga) huchangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa imani potofu zinazoshawishi matendo ya kinyama dhidi ya albino.
Kadhalika, njia nyingine nzuri ni kuwatumia watu waliowahi kukamatwa na viungo vya albino na kuwabana zaidi ili wawataje wateja wao wakuu ambao nao watapaswa kushughulikiwa ipasavyo, bila kujali umaarufu wao wala ukwasi wao.
Aidha, elimu iendelee kutolewa kila uchao kuhusiana na ukweli kwamba albino hawana tofauti na watu wengine. Muonekano wa ngozi zao ni matokeo ya sababu za Kibaiolojia na wala hakuna uhusiano wowote wa viungo vyao na mafanikio ya mtu yeyote kimaisha.
Wanastahili upendo na haki nyingine zote za binadamu. Ni ujinga mkubwa kuamini kuwa eti, kiungo cha albino kinasaidia mtu kupata madini mengi migodini, kupata nafasi za uongozi, mafanikio katika biashara, ufugaji, kilimo, uvuvi au shughuli yoyote ya kiuchumi.
Shime, kasi iongezwe kuwakomboa watoto hawa waliotekwa na pia kuwanasa wahusika wote wa vitendo hivi vilivyokosa chembe ya utu.
CHANZO: NIPASHE