Thursday, February 19, 2015

Escrow yapasua CCM: WAZEE WA MKOA WA KAGERA KUJIVUA CCM...Tayari wazee hao, wako jijini Dar kuonana na rais kupinga Prof. Tibaijuka “kufanywa mbuzi wa kafara



Escrow yapasua CCM: WAZEE WA MKOA WA KAGERA KUJIVUA CCM...Tayari wazee hao, wako jijini Dar kuonana na rais kupinga Prof. Tibaijuka "kufanywa mbuzi wa kafara
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya              Kikwete (katikati) akiongoza kikao cha NEC, Kulia ni Katibu              Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana na kushoto ni Makamu, Ali              Mohamed Shein
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete (katikati) akiongoza kikao cha NEC, Kulia ni Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana na kushoto ni Makamu, Ali Mohamed Shein

SAKATA la ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi ndani ya Benki Kuu (BoT), limeanza kukipasua Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tayari wazee na viongozi wa chama hicho kutoka mkoani Kagera, wametishia kuondoka chama hicho kwa madai ya unyanyasaji dhidi ya wananchi wa mkoa wa Kagera." 

Hatua ya viongozi hao, inafuatia kuwapo taarifa kuwa chama hicho, kimepanga kumfukuza katika Kamati Kuu (CC), Prof. Anna Tibaijuka.
Tayari wazee na viongozi hao, wako jijini Dar es Salaam kuonana na rais kupinga Prof. Tibaijuka "kufanywa mbuzi wa kafara."
Prof. Tibaijuka alifukuzwa kazi na Rais Kikwete mwishoni mwa mwaka jana. Ametajwa kuwa miongoni mwa walionufaika na mgawo wa Sh. 1.6 bilioni kutoka kwa James Rugemalira, mmoja wa waliokuwa wamiliki wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Rugemalira alikuwa akilimiki asilimia 30 ya hisa katika IPTL, kupitia kampuni yake ya VIP Engineering and Marketing Limited.
Mmoja wa viongozi katika ujumbe huo ametuambua kuwa kumfukuza Prof. Tibaijuka ni mkakati wa kuengua viongozi kutoka mkoa wa Kagera; na kuonya kuwa Tibaijuka akifukuzwa CC, basi chama hicho kisitegemee kupata "hata kiti kimoja cha ubunge" mkoani Kagera.

Prof. Tibaijuka ni mbunge wa Muleba Kusini (CCM). Alikuwa waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Ni mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa mkoani humo.

Taarifa zinasema, mkakati wa kumfukuza kazi Prof. Tibaijuka, kuondolewa kwenye kamati kuu na baadaye kufikishwa mahakamani, unasukwa kwa ustadi mkubwa na waziri mmoja mwandamizi katika serikali ya Rais Kikwete.

Katika jitihada za kutaka kujiondoa katika dimbwi la lawama, mtoa taarifa anasema, baadhi ya maafisa waandamizi wa ikulu wamemshauri Rais Kikwete kumtosa Prof. Tibaijuka, ili kulainisha nchi wahisani.

Mtoa taarifa anasema, mmoja wa mawaziri katika serikali ya Rais Kikwete, aliwasilisha pendekezo kwa rais kuwa Tibaijuka ana sifa kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo akifukuzwa kazi dunia nzima itaona kuwa "serikali iko makini."

Amesema washauri walidai kuwa kufukuzwa kazi kwa Prof. Tibaijuka kutazima sakata zima la Escrow; kwani kusingekuwa tena na kelele za wahisani; na misaada yote ingerejea na hali kuwa kama awali.

Viongozi wanaotajwa kutinga jijini, wanaongozwa na Pius Ngeze, mwenyekiti mstaafu wa chama hicho mkoani Kagera; Costancia Buhiye, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho mkoani Kagera na Ally Ameiry, katibu wa CCM mkoani.
Wengine walioko jijini kukabiliana na wanaotaka kumuondoa Prof. Tibaijuka katika kamati kuu, ni Faustine Kamaleki, Sebastian Rwitelana, ambaye ni diwani wa kata ya Nshamba na Zaidia Juma, katibu wa tawi la Bujumbi.
Taarifa za awali zilisema ujumbe huo umeshikilia kwamba, kwa kuwa rais alisema fedha za Escrow ni mali ya mtu binafsi, hakukuwa na sababu ya kumgeuza Prof. Tibajuka kuwa "mbuzi wa kafara."
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, hatua ya viongozi hao kujitosa kumtetea Prof. Tibaijuka, imekupasua chama hicho. Hii inatokana na udhaifu wa Rais Kikwete katika kushughulikia suala hilo.
"Wako wapi wezi wa Escrow katika akaunti ya Stanbic? Hakuna anayejadili hilo. Badala yake, viongozi wa CCM wanahaha kuhangaika na Tibaijuka, aliyepewa fedha na ndugu yake," ameeleza mmoja wa viongozi serikalini.