Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda(pichani), ameunga mkono 'mwendo wa kinyonga' unaofanywa na Serikali kuhamishia makao Makuu ya nchini mkoani Dodoma.
Alitoa kauli hiyo bungeni jana baada ya Naibu wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Agrey Mwanri kujibu swali la Mbunge wa Chilonwa (CCM), Hezekia Chibulunje kutaka kujua sababu za mswada wa kutambua Dodoma kuwa makao makuu ya nchi kuchelewa kuwasilishwa bungeni.
Mwanri alisema utekelezaji wa sheria ya kutambua Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, ikiwamo ukomo wa muda ambao Serikali itahamia utawekwa kwa utaratibu mahsusi, kupitia kanuni zitakazotungwa na Waziri mwenye dhamana ya Ustawishaji Makao Makuu.
Alisema kwa sasa Waraka wa Baraza la Mawaziri wa kutunga Sheria hiyo, uko katika hatua ya kupata maoni ya sekretarieti yake hivyo bado kuna hatua mbili katika mfumo wa kuandaa muswada huo kabla ya kuwasilishwa bungeni.