Monday, February 02, 2015

Bunge kujadili ripoti za CAG



Bunge kujadili ripoti za CAG
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo linaingia awamu ya pili na ya mwisho ya mkutano wake wa 18, ambao pamoja na mambo mengine, unatarajia kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
 
Taarifa hizo za CAG ziliwasilishwa katika mkutano wa Bunge wa 15 uliofanyika Aprili, mwaka jana.
 
Pia wabunge wanatarajia kujadili na kupitisha muswada unaopendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara, unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju.
 
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema jana kuwa hakuna mabadiliko yoyote ya ratiba ya shughuli za mkutano wa sasa wa 18 wa Bunge iliyotolewa Jumatatu ya wiki iliyopita.
 
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya, taarifa hizo za CAG zitajadiliwa na wabunge kwa siku mbili mfululizo.
 
Taarifa hizo zinahusu hesabu zilizokaguliwa za serikali kuu, serikali za mitaa na mashirika ya umma.
 
Mbali na taarifa hizo, pia taarifa za Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji zitajadiliwa.
 
Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya Bunge, taarifa za kamati hizo zitajadiliwa Februari leo, kesho na keshokutwa.
 
Ratiba hiyo pia inaonyesha kuwa wabunge watajadili pia taarifa za kamati ya Katiba, Sheria na Utawala; ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ya Masuala ya Ukimwi.
 
Taarifa nyingine zitakazojadiliwa ni za Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara.
 
Pia miswada miwili itasomwa na kupitishwa na wabunge ukiwamo wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2014 na ule wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa mwaka 2014.
 
Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa 2014, pamoja na mambo mengine, unapendekeza marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964.
 
Kwa mujibu wa Masaju, marekebisho ya sheria hiyo ya Tamko la Sheria ya Kiislamu, unapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.