Monday, February 02, 2015

Mwanasheria Mkuu wa serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wamepandishwa kizimbani kwa kuvuruga uchaguzi



Mwanasheria Mkuu wa serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wamepandishwa kizimbani kwa kuvuruga uchaguzi
Mwanasheria wa Serikali, George Masaju.

Mwanasheria wa Serikali, George Masaju, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, Meleckzedeck Humbe, wamepandishwa kizimbani, wakikabiliwa na mashtaka ya ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Desemba 14, mwaka jana.
 
Masaju na wenzake, wanakabiliwa na kesi namba 04 ya mwaka 2015 iliyofunguliwa na Gerald Mlay katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai, akipinga matokeo yaliyotangazwa na kumpa ushindi mpinzani wake, Peter Mshiko (CCM) ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Orori, Kata ya Narumu.
 
Mwanasheria Mkuu pamoja na Mkurugenzi wa Wilaya ya Hai, waliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Leah Kimaro, ambaye alimwomba Hakimu Mkazi Mfawidhi, Denis Mpelembwa, kumpa siku 14 za kuandika majibu ya shtaka linalowakabili.
 
Kwa mujibu wa wakili huyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hai, hajampa taarifa ya kimaandishi kuhusu uchaguzi unaodaiwa kutokuwa huru na haki.
 
"Ikikupendeza mheshimiwa, naomba nitoe udhuru wa Mkurugenzi wa Upepelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DPP), kwamba hakuweza kufika mahakamani hapa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, lakini pia naomba mahakama yako tukufu inipe muda wa siku 14 za kuandika majibu," alidai wakili huyo. Baada ya ombi hilo, Hakimu Mpelembwa alisema kwa kuwa upande wa Jamhuri, umeomba muda wa kuandika majibu, mahakama, hivyo mahakama imeridhia na kwamba kesi hiyo itatajwa tena Februari 16, mwaka huu.
 
Mbali na kesi hiyo, Humbe na baadhi ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo, bado wanakabiliwa na kesi nyingine tano za uchaguzi zilizofunguliwa mahakamani hapo.
 
Kwa mujibu wa kalenda ya mahakama hiyo, atapandishwa tena kizimbani Februari 5, mwaka huu.
 
Mara baada ya kuahirishwa kwa shauri hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Rashid Kitambulilo na wenzake wawili, nao walipandishwa kizimbani, wakikabiliwa na kesi namba 06 ya mwaka 2015 ya ukiukwaji wa taratibu na kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa wa Desemba 14, mwaka 2014.
 
Walalamikaji katika kesi hiyo, Richard Maly na wenzake 44 ambao ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Siha ambao wamefungua kesi,  wakidai uchaguzi huo uligubikwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa Serikali za Mitaa.