Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda (pichani), inaendelea tena leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro kwa shahidi wa tatu kutoa ushahidi wake kati ya mashahidi 15 wa upande wa mashtaka wanaotarajia kutoa ushahidi.
Kesi ilianza kusikilizwa Januari 26, mwaka huu mbele ya hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Mary Moyo imekuwa ikivutia wengi kujitokeza katika Mahakama hiyo wakiwemo wafuasi wa kiongozi huyo.
Katika kesi hiyo Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kutotii amri halali ya Mahakama, kutoa maneno yenye nia ya kuharibu imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa ambayo yote hayo anadaiwa kuyatenda Agosti 10 mwaka 2013 katika uwanja wa Shule ya msingi Kiwanja cha ndege Manispaa ya Morogoro.
Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ni aliyekuwa mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro (OCD) Sadick Tindwa ambaye kwa sasa ni mkuu wa polisi Wilaya ya Handeni, Tanga na shahidi wa pili ni aliyekuwa Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Morogoro (RCO) Jafert Kibona (sasa ni Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Mtwara).
Licha ya mashahidi hao Wakili wa upande wa Serikali Benard Kongola aliieleza mahakama kuwa vipo vielelezo vitakavyotolewa mahakamani hapo ambapo mpaka sasa tayari kimeshatolewa kielelezo kimoja ambacho ni kibali cha kuruhusu kufanyika kwa kongamano la Eid pili ya mwaka 2013 ambacho kilitolewa na shahidi wa kwanza.
Pamoja na kesi hiyo kuendelea kusikilizwa Sheikh Ponda bado yuko rumande kutokana na mahakama hiyo kushindwa kumpa dhamana kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na hati iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo kwa maslahi ya Taifa.