Mwili huo uligundulika majira ya saa sita mchana baada ya watu waliopita katika eneo hilo kuuona ukiwa umelazwa karibu na moja ya shamba lililopo mtaa wa Bunkango eneo la kambi hiyo ya Polisi.
Paparazi ilishuhudia mwili huo ulioanza kuharibika ukiwa umevuliwa nguo zote ukiwa bado haujaondolewa katika eneo hilo la tukio.
Mwili huo ulikuwa na majeraha maeneo ya usoni kiasi cha kushindwa kutambulika kirahisi.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, Kaimu Mtendaji wa kata ya Nshambya, Christian Ngaiza, alisema alipata taarifa za tukio hilo kutoka kwa dereva wa bodaboda kuwa kuna mtu ameuawa lakini wananchi wanaogopa kutoa taarifa Polisi.
Ngaiza, alisema baada ya kupata taarifa hiyo aliamua kwenda eneo la tukio majira ya saa saba mchana na kutoa taarifa ya tukio hilo Polisi.
Aidha, alisema baada ya kubaini mwili huo, alianza uchunguzi na kuhoji wananchi wa mitaa yote mitatu ya eneo hilo endapo wana taarifa za mtu yeyote aliyepotea ambapo ilibainika hakukuwa na mtu aliyepotea.
Mkazi wa Mtaa wa Migera, Joyce Nuru, akizungumzia tukio hilo, alisema alipata taarifa za kukutwa kwa maiti huyo, akiwa nyumbani kwake ambapo majira ya saa sita mchana wanafunzi walipita na kumueleza kuwa kuna mtu amekufa maeneo ya mnara.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera ambaye pia ni mpelelezi wa makosa ya jinai mkoani humo, Gilles Mroto alisema tukio hilo amelisikia na ametuma timu ya maofisa wa Polisi kwenda eneo la tukio kufanya uchunguzi.
Hata hivyo, mwili huo haukuweza kutambulika na hivyo kuzikwa na Manispaa ya Bukoba katika makaburi ya Kyebitembe.