Sunday, January 04, 2015

JKT KANEMBWA YAIOMBA HALMASHAURI YA KIGOMA KUMALIZA MCHAKATO WA KUKIPATIA HATI MILIKI YA MAENEO YA KIKOSI




JKT KANEMBWA YAIOMBA HALMASHAURI YA KIGOMA KUMALIZA MCHAKATO WA KUKIPATIA HATI MILIKI YA MAENEO YA KIKOSI
Na Editha Karlo wa Globu ya Jamii,Kigoma

KAMANDA wa Kikosi cha Jeshi la kujenga Taifa (JKT) 824 KJ cha Kanemwa wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma Luteni Kanali Erasmus Bwegoge ameomba Halmashauri ya wilaya hiyo kutilia mkazo na kuhitimisha mchakato wa kupata hati miliki ya maeneo ya kikosi hicho ili kuondoa uwezekano wa wananchi kuvamia maeneo hayo jambo ambalo linaweza kuzua migogoro na kuhatarisha mahusiao baina ya Jeshi na wananchi.

Luteni kanali Bwegoge ametoa ombi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni kanali mstaafu Issa Machibya wakati wa mahafali ya nne ya kuhitimu mafunzo ya jeshi kwa mujibu wa sheria .

''Mgeni rasmi tunaomba Halmashauri yetu ya Kakonko suala la kupata hati miliki ya maeneo ya kikosi chetu hiki,hii itatusaidia sana kuondoa migogoro ya ardhi baina ya wananchi na jeshi,pia itasadia kutokuwepo na wananchi wanaovamia katika maeneo ya jeshi''alisema.

Alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa changamoo hiyo ya ardhi kikosini hapo pia kuna changamoto za huduma bora za afya alisema jumla ya vijana 1127 wa oparesheni ya miaka 50 ya muungano wamehitimu mafunzo hayo ambao ni wahitimu wa kozi ya ualimu na wale waliomaliza kidato cha sita .

Kwa upande wake mwakilishi wa mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa nchini(JKT) Meja Abdulrahmani Dachi na mgeni rasmi katika maafali hayo Mkuu wa M koa wa Kigoma Luten Kanali mstaafu Issa Machibya wamewataka vijana hao kutumia mbinu walizojifunza kudumisha ulinzi na usalama wa nchi pamoja na kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jamii na si kulihujumu Taifa kwa namna yeyote.

''Muende mkawe mfano wa kuigwa katika jamii pia mtumie mbinu mlizofundishwa katika kudumisha ulinzi na usalama wa nchini pia mkawe mfano katika shughuli za maendeleo katika jamii''alisema Mkuu wa Mkoa
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa katika kikosi cha 824 KJ Kanembwa wakiwa tayari kwaajili ya Gwaride.
Wahitimu wakipita mbele ya mgeni (hayupo pichani)Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali mstaafu Issa Machibya rasmi kwa mwendo wa pole.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya akiwa amesimama kwa ukakamavu wimbo wa Taifa ukiimbwa kwaajili ya ufunguzi wa sherehe za maafali ya kufunga mafunzo ya JKT katika kikosi cha 824KJ Kanembwa.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya JKT kikosi cha 824 KJ wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi katika maafali yao ya kufunga mafunzo.
(picha zote na Editha Karlo)