Na JOHN DOTTO, Mwanza
WAZIRI wa Ujenzi Dkt. John Magufuli ameagiza kufungwa kwa mfumo mpya wa kielektroniki katika vivuko vyote nchini ili kukabiana na wajanja wachache wanahujumu mapato katika vivuko hivyo.
Mbali ya hilo, ameagiza kufanywa kwa utaratibu utakaowezesha huduma katika vivuko zinatolewa kwa saa 24 ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Dkt. Magufuli alitoa maagizo hayo jana katika uzinduzi wa mfumo mpya wa kielektroniki katika kivuko cha Kigongo -busisi mkoani hapa uliowekwa na Kampuni ya Africom Tanzania.
"Tulianze pale Kigamboni na tukaona mafanikio, tulipokuja hapa (Kigongo) tukaboresha na mafanikio yameonekana kwa kiasi kikubwa. Vivuko vyote sasa vifungwe mfumo mpya wa kielektroniki...vivuko vyote nchini," aliagiza Dkt. Magufuli.
Alisema mfumo huo una faida kubwa ikiwemo kudhibiti upotevu wa mapato ambapo katika kivuko cha kigongo - Busisi alisema mapato yameongezeka kwa takribani asilimia 40 baada ya kufungwa kwa mfumo huo.
Hata hivyo, Dkt. Magufuli alikataa kutaja ni kwa shilingi ngapi mapato hayo yameongezeka kwa hofu kuwa watu wenye dhmira mbaya wakisikia wanaweza kwenda na kufanya uhalifu.
Pia, aliagiza Kivuko kwa Kigamboni nacho kiboreshwe mfumo wake kama ilivyokuwa kwa Kigongo - Busisi. Waziri huyo wa Ujenzi, alisema kutokana na mafanikio yanayopatikana katika kudhibiti upotevu wa mapato na kurahisisha huduma kwa wananchi, wafanyakazi husika kwa maana ya wale wa TEMESA maslahi yao yanapaswa kuangaliwa upya na kuboreshwa. "Kama mapato ni mazuri, wafanyakazi nao walipwe vizuri, wasikae kimasikini kwani wanapaswa kuona mwaka 2015 ni ukombozi katika maisha yao.
Alisema serikali chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete imefanikiwa kujenga madaraja yote makubwa nchini ambapo kwa sasa kuna madaraja 4880 nchini na kuwa wakati inapata uhuru kulikuwa na madaraja mawili ambayo yalikuwa ya kuvutwa.
Mfumo wa kielektroniki katika vivuko vya Kigamboni na Kigongo Busisi ulifungwa na Kampuni ya Africom Tanzania ambaye Mkurugenzi Mtendaji wake Juma Rajabu alisema watahakikisha wanafunga mifumo ambayo itadhibiti upotevu wa mapato na kurahisisha huduma kwa wananchi ambao ndiyo watumiaji.
Dkt. John Magufuli akikata utepe kuzindua mfumo mpya wa kielektroniki katika kivuko cha Kigongo -busisi mkoani hapa uliowekwa na Kampuni ya Africom Tanzania.
Dkt. John Magufuli akikata utepe kuzindua mfumo mpya wa kielektroniki katika kivuko cha Kigongo -busisi mkoani hapa uliowekwa na Kampuni ya Africom Tanzania.
Dkt. John Magufuli na viongozi wa mkoa wa Mwanza wakifurahia baada ya kukata utepe kuzindua mfumo mpya wa kielektroniki katika kivuko cha Kigongo -busisi mkoani hapa uliowekwa na Kampuni ya Africom Tanzania.
Mfanyakazi wa kivuko cha Kigongo -busisi mkoani Mwanza akionesha wananchi namna ya kutumia mashine hiyo