Tuesday, January 27, 2015

Baba mzazi ampiga kichanga cha mwezi kwa mchi kichwani, ni katika ugomvi



Baba mzazi ampiga kichanga cha mwezi kwa mchi kichwani, ni katika ugomvi
Mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja, Yadiko Chigoda amelazwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma baada ya kupigwa na mchi kichwani na baba yake mzazi na kumsababishia maumivu makali.
Akizungumza na paparazi mama mzazi wa mtoto huyo, Carolina Mnyawami  mkazi wa Kijiji cha Mingui Kata ya Lumuma wilayani hapa alisema, tukio hilo limetokea jana saa 4 asubuhi wakatimume wake Fabian Chigoda alipokuwa akipigana na kaka yake kwa kuchapana fimbo na yeye aliamua kuwaamulia ugomvi huo.
"Nilipowanyang'anya fimbo ili wasiendelee kupigana, mume wangu aliokota mchi na kunirushia kichwani... Niliukwepa ili usinipige ndipo ulipompiga kichwani mwanangu niliyekuwa nimembeba mgongoni," alisema Carolina.
Aliongeza kuwa, "Baada ya kuona kuwa amempiga mtoto alikimbia na hajulikani alipo mpaka sasa."
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Said Mawji amethibitisha kumpokea mtoto huyo na kwamba kwa sasa anaendelea kupatiwa uchunguzi zaidi wa afya yake.
"Mtoto huyo aliumia sana kichwani lakini bado tunampatia tiba na uchunguzi zaidi kwenye fuvu la kichwa, kwani inaonekana kama vile limepasuka."
Hata hivyo, alisema wanafanya mpango wa kumpa rufaa mtoto huyo ili aweze kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mingui, Mwingwa Udoba alisema chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia na kwamba bado wanamtafuta baba mzazi wa mtoto huyo kwa kuwa alikimbia baada ya tukio hilo.
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alipotafutwa simu yake ilipokewa na mtu aliyesema yuko kwenye kikao cha kazi.