Wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuanzia mwaka 2000 hadi 2014, wanatarajia kuandamana tena keshokutwa kwenda Ikulu jijini Dar es Salaam kuwasilisha kilio chao cha kukosa ajira kwa muda mrefu.
Vijana hao wameamua kuandamana kwenda kuwasilisha kilio chao hicho kwa Rais Jakaya Kikwete baada ya kuandika barua tatu kwenda Ikulu bila kujibiwa.
Akizungumza kwenye mkutano wa vijana hao Mwenyekiti wa Umoja huo, George Mgoba, alisema vijana wengi wamekuwa wakipelekwa kwenye mafunzo ya JKT na kuahidiwa kupatiwa ajira na serikali huku wakiishia mitaani.
"Jumatano tutaandamana kwenda Ikulu kumuona Rais na kumfikishia kilio chetu cha kukosa ajira kwa miaka yote hiyo kwani tunaamini wanaomwakilisha wanamdanganya kwa kudai kuwa vijana wote waliomaliza JKT wameajiliwa sehemu mbalimbali kitendo ambacho siyo,"alisema Mgoba
Alihoji sababu za serikali kuwapeleka vijana kwenye mafunzo hayo wakati haina uwezo wa kuwaajiri.
Mgoba alisema chakushangaza JKT hiyo hiyo inaajiri vijana wanaotoka visiwani Zanzibar lakini wanaotoka Bara wanarudishwa nyumbani.
Alisema hata ajira ambazo zimekuwa zikitolewa ni kwa upendeleo na kwa vijana wasio na sifa kitendo ambacho hakiwatendei haki.
Vijana hao waliandamana Desemba17, mwaka jana kwenda Ikulu kuonana na Rais Kikwete lakini Jeshi la Polisi Kanda Maalumu jijini Dar es Salaam liliwazuia na kuwataka kuteua viongozi watano wa kuwasilisha malalamiko yao.
Hata hivyo, hawakufanikiwa kuonana na Rais Kikwete na baadala ya kukutana na wasaidizi wake.