JANA Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilisema itaanzisha bahati nasibu ili kuhamasisha Watanzania, kujenga utamaduni wa kuomba risiti pindi wanaponunua bidhaa mbalimbali. Ushawishi huo ni sehemu tu ya juhudi ya kutaka kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania, wanasaidia serikali katika kufanikisha makusanyo ya mapato.
Kwa wale wanaojua kwamba ili serikali ifanye kazi ni lazima iwe na mapato, wataunga mkono hatua hii ambayo ni muhimu, kwani itatambulisha pia kwanini serikali inahitaji fedha hizo za risiti.
Pamoja na taarifa hizo za kufurahisha ni jambo la kusikitisha kuona kwamba taasisi inalazimika kuanzisha bahati nasibu, kama sehemu ya kutengeneza mwamko wa wananchi kuhusu mapato ya serikali.
Kukosekana kwa utamaduni wa kudai risiti, kumefanya mapato ya serikali kupotea na hivyo kuikosesha nguvu ya kusaidia wananchi wake katika masuala ambayo serikali lazima iyatende.
Watanzania kwa ujumla wao, wanapaswa kuamka na kujisifia kwa kulipa kodi au kuiwezesha serikali kukusanya kodi yake kwa kutokubali kushawishika kwenda kinyume na taratibu za ulipaji kodi.
Kama tutatambua kwamba serikali shamba lake ni kodi, tukasaidia kodi hiyo ikalipwa, tutakuwa tunaongeza uwezo wa serikali kutoa huduma nyingine kama ununuaji wa dawa, utengenezaji wa barabara, utengenezaji wa miundombinu na hata kuiwezesha elimu ikawa ya bure.
Tunapenda kuamini kwamba juhudi zinazofanywa na Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi ya TRA zitafanikiwa. Ni kweli, kwa jinsi tulivyo Watanzania, huenda bahati nasibu hiyo na kampeni kubwa ya kutambua umuhimu wa kodi, vitasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Kwa nia njema tunawasihi Watanzania kusaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato, kwani watu watashawishika kutafuta faida ya ununuzi wao kwa kushiriki bahati nasibu hiyo kwa kuchukua risiti zao. Tunawasihi Watanzania kushiriki kwa wingi katika bahati nasibu hiyo kwa kudai risiti.
Tunapenda kuwaomba wananchi kutambua kwamba upotevu wa mapato ni suala hatari kwa taifa la kwetu, ambalo msingi wa huduma kwa jamii unategemea zaidi serikali. Wananchi tusipopunguza tatizo hilo, tutaifanya serikali kushindwa kutekeleza wajibu wake wa msingi kwa wananchi wa Tanzania, kuimarisha huduma za jamii na kuweka sawa miundombinu stahiki kwa ajili ya ukuzaji uchumi.
Kutokana na ukweli huo, tunawapongeza wote wanaojitahidi kushawishi wananchi kutambua wajibu wao katika maendeleo yao, mfano wajibu huo wa kudai risiti ili kuwalazimisha wafanyabiashara kuacha kuiibia serikali.
HABARI LEO.