Mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema iwapo atachaguliwa katika nafasi hiyo, atahakikisha kwamba serikali yake inawafutia mikopo wanafunzi wote wa elimu ya juu waliowahi kukopeshwa kwa ajili ya masomo ya vyuo vikuu.
Lowassa anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro jana.
Alisisitiza kuwa serikali yake atakayoiunda, itatoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu na kwa wale ambao tayari wanadaiwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, watafutiwa kiasi chote wanachodaiwa.
Alisisitiza kuwa serikali yake atakayoiunda, itatoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu na kwa wale ambao tayari wanadaiwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, watafutiwa kiasi chote wanachodaiwa.
"Serikali yangu itatoa elimu kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu bure na wanaodaiwa na Bodi, tutawafutia mikopo yao," alisisitiza Lowassa.
Kuhusu tatizo la umeme kukatika mara kwa mara, Lowassa alitoa onyo kwa watendaji wa Tanesco kuwa akiingia madarakani wajiandae kutafuta kazi nyingine kwa kuwa umeme umekuwa ni kero kwa wananchi kutokana na kukatika mara kwa mara pasipo sababu za msingi.
"Uchumi unasimama kwa kukosekana umeme wa uhakika, uwezo upo lakini viongozi wetu wameshindwa kulitatua," alisema Lowassa na kuongeza:
"Ninawaambia Tanesco wajipange baadhi ya watendaji watafute kazi nyingine."
Alisema bila kufanyika uamuzi wa haraka kutatua tatizo la umeme nchini mambo mengi yanakwama na uzalishaji viwandani unadorora na gharama za bidhaa kupanda hivyo kumuumiza mwananchi wa kawaida.
Aidha, akiwa katika Wilaya ya Mwanga ,mkoani Kilimanjaro, Lowassa alisema serikali yake itahakikisha huduma ya maji inapatikana wilayani humo kwa asilimia 100.
Alisema anashangaa kuona wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo la maji kwa miaka mingi, lakini yeye atalimaliza katika uongozi wake.
Wakati huo huo, Lowassa jana alitembelea kaburi la aliyekuwa muasisi wa Tanu na baadaye CCM, marehemu Peter Kisumo.
Kisumo alifariki dunia Agosti 3, mwaka huu na kuzikwa kijijini kwao Usangi wilayani Mwanga ambapo wakati wa mazishi, Lowassa hakuhudhuria kwenye mazishi ya Kisumo baada ya msafara wake kuzuiwa na polisi.
Lowassa, ambaye aliongozana na aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, mgombea wa Vunjo, James Mbatia na mgombea wa Mwanga, Henry Kileo, walipokelewa na kaka wa marehemu, Daniel Mchangila.