Monday, October 05, 2015

Tanesco tunapata hasara Sh. milioni 500 kila siku kutokana na kukatikatika kwa umeme..Suala hilo halihusiani na siasa


Tanesco tunapata hasara Sh. milioni 500 kila siku kutokana na kukatikatika kwa umeme..Suala hilo halihusiani na siasa

Mbali na umeme wa gesi, hali ya mabwawa yanayozalisha umeme kwa sasa hayana maji ya kutosha na baadhi yanaelekea kukauka.
Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limesema linapata hasara ya Sh. milioni 500 kila siku kutokana na kukatikatika kwa umeme.
 
Aidha, Tanesco imesema tatizo la kukatikakatika kwa umeme ni la kiufundi na si kwa lengo la kuwakomoa wananchi.
 
 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felichesmi Mramba, alisema hali ya kukatika kwa umeme inayoendelea nchini inatokana na marekebisho ya baadhi ya mitambo ya kuzalisha umeme na mifumo ya gesi inayomilikiwa na kampuni binafsi.
 
Alisema hali hiyo inakwamisha upatikanaji wa huduma ya nishati hiyo.  "Suala hilo halihusiani na siasa, bali ni matatizo ya kitaalam ambayo hata shirika linapata hasara," alisema.
 
"Baada ya bomba la gesi kukamilika, visima viwili kati ya vinne vilianza kuingiza gesi kwenye bomba Agosti 22, mwaka huu kule Mtwara na ilifika jijini Dar es Salaam Septemba 5, mwaka huu … hata hivyo, gesi hiyo ilifika ikiwa na msukumo mdogo na ilichukua wiki mbili kufikia kiwango cha  kuwezesha kuwasha mitambo ya megewati 90," alisema na kuongeza:
 
"Mtambo wa Kinyerezi kazi inaendelea hadi wataalam watakaporidhika kwamba mabomba yote ni masafi na yanaweza kuanza kuwashwa tayari kwa kutoa huduma… kukamilika kwa mitambo hiyo kutatuhakikishia jumla ya megawati 305 zaidi ya umeme unaopatikana sasa," alisema  Mramba.
 
" Mbali na umeme wa gesi, hali ya mabwawa yanayozalisha umeme kwa sasa hayana maji ya kutosha na baadhi yanaelekea kukauka," alisema.
 
 Alitaja mabwawa hayo na kiwango chake cha maji kuwa Mtera uwezo wake wa juu ni megawati 800, uzalishaji wake wa sasa ni sifuri, Kidatu megawati 204, lakini sasa linazalisha megawati 27, Kihansi (megawati (180) sasa linazalisha megawati 51.5, New Pangani Falls (megawati 68), lakini kwa sasa linazalisha megawati 17, Hale  (megawati 21), sasa megawati nne na Nyumba ya Mungu uwezo wake ni kuzalisha megawati nane, lakini kwa sasa linazalisha megawati 5.5.
 
 Alisema shirika linasikitishwa na taarifa za uzushi zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii kwamba mitambo ya Kinyerezi ni chakavu haiwezi kufanya kazi kwamba zimelenga kulichafua shirika hilo.