Sunday, December 07, 2014

WAMA KWA KUSHIRIKIANA NA ENGENDERHEALTH KWA UFADHILI WA WATU WA MAREKANI KUZINDUA KAMPENI YA KUZUIA MIMBA ZA UTOTONI




WAMA KWA KUSHIRIKIANA NA ENGENDERHEALTH KWA UFADHILI WA WATU WA MAREKANI KUZINDUA KAMPENI YA KUZUIA MIMBA ZA UTOTONI
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kushirikiana na Engenderhealth kwa ufadhili wa watu wa Marekani itazindua kampeni ya kuzuia mimba za utotoni katika Shule za Sekondari ijulikanayo kama  "Jilinde Utimize Ndoto Yako" kesho Jumatatu tarehe 08 Desemba,  2014. 

Uzinduzi huo utafanyika katika viwanja vya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kuanzia saa 4.00 Asubuhi hadi 07.00 Mchana. Mgeni Rasmi atakuwa Mhe. Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA. 
Lengo la kampeni hii ni kuongeza uelewa  na stadi juu ya masuala ya afya ya uzazi kwa vijana wa kike ili wajikinge na mimba za utotoni, UKIMWI na tabia hatarishi  hatimaye wamalize masomo yao salama. 
Tamasha la uzinduzi huu litajumuisha wanafunzi wa kike zaidi ya 200 na walimu wao kutoka Wilaya ya Temeke na Shule za Jirani. Viongozi mbalimbali wa serikali na watendaji wa asasi zisizo za kiserikali  zinazoshughulikia masuala ya vijana pia wanatarajiwa kuhudhuria.
Kuanzia mwaka 2010- 2012 mradi wa kuwajengea wanafunzi stadi za afya ya uzazi ili kujikinga na mimba za utotoni ulitekelezwa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kufanya shughuli zifuatazo; Kutoa mafunzo ya afya ya uzazi na stadi za maisha kwa vijana wa kike walio katika shule za sekondari, kuelimisha jamii na wazazi kupitia matamasha ya kijamii na kutengeneza na kusambaza zana za upashaji habari na mawasiliano. Kwa mwaka huu wa 2014 Mradi huu utatekelezwa Mkoa wa Dar es Salaam Wilaya ya Temeke pamoja na kufanya ufuatiliaji wa Maendeleo ya Mikoa mingine ambapo mradi unatekelezwa. 
Mradi huu umefadhiliwa na Watu Wa Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na kutekelezwa na Shirika la Engenderhealth na Taasisi ya WAMA. 
TAASISI YA WANAWAKE NA MAENDELEO (WAMA) ilianzishwa mwaka 2006 na Mhe. Mama Salma Kikwete, Mke wa Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania. WAMA ni Taasisi isiyo ya kiserikali yenye lengo la kuwaendeleza wanawake na wasichana wa Kitanzania katika Nyanja za elimu, afya  na uchumi hasa waliotoka katika mazingira hatarishi