Tuesday, December 23, 2014

BOMA LA MJERUMANI KUJENGWA MAKUMBUSHO



BOMA LA MJERUMANI KUJENGWA MAKUMBUSHO


Chuo  Kikuu Iringa (UOI), kinatarajia kuanza ukarabati wa jengo la kale lilojengwa na Serikali ya Ujerumani enzi za ukoloni linalojulikana kama Boma lililopo mkoani hapa. 



UOI kinakarabati jengo hilo kupitia mradi wa kuendeleza utamaduni nyanda za juu kusini uitwao Fahari Yetu kwa kushirikiana na wadau wake, Wizara ya Maliasili na Utalii Idara ya Mambo ya Kale, Makumbusho ya Taifa  na ofisi ya mkuu wa mkoa Iringa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Hosea Mpogole kwa niaba ya mkuu wake,  Profesa Nicholas Bangu, alisema kuwa mradi huo wa kitalii utakaogharimu  mamilioni ya shilingi za Kitanzania, utahusisha ukarabati, uhifadhi na uhuishaji wa boma hilo.

Alisema makubumsho ni kati ya maeneo bora  duniani ya kujifunzia, kufanya maonyesho ya mambo ya kisayansi kama uvumbuzi, kazi za sanaa na za kihistoria na ni kituo muhimu kwa ajili ya utafiti, matamasha ya asili na ushawishi.

Alisema chuo hicho kimejikita kutoa uwezo wa kitaaluma ambao utatoa fursa ya kufundisha kwa vitendo badala ya kuwa na nadharia pekee.

 " Mradi huu wa Fahari Yetu umetenga fedha kwa kubadilisha Boma la Mjerumani na kulifanya kuwa jengo la makumbusho ya urithi wa kiutamaduni. Mradi huu makao makuu yake yatakuwa Chuo Kikuu Iringa," alisema Dk. Mpogole.

Alisema chuo hicho kinapitia upya na kuboresha mtaala wake wa idara ya utamaduni na utalii ili kuboresha kozi hiyo na utafiti katika kuhakikisha taaluma inaunganisha shughuli za urithi wa mambo ya asili, utamaduni na uhifadhi kwa ajili ya kukuza sekta ya utalii Nyanda za Juu Kusini na taifa.

 Katibu wa Tawala wa Mkoa wa Iringa, Ayub Wamoja kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Juma Masenza,  alisema kuwapo kwa makumbumsho ndani ya mkoa kutakuza kwa kiwango kikubwa sekta ya utalii ndani ya nchi kwa kuongeza thamani ya vivutio.
CHANZO: NIPASHE