Saturday, December 13, 2014

TANZANIA YAISHAURI MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA MAKOSA YA JINAI (ICC) KUBORESHA UHUSIANO WAKE NA BARA LA AFRIKA




TANZANIA YAISHAURI MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA MAKOSA YA JINAI (ICC) KUBORESHA UHUSIANO WAKE NA BARA LA AFRIKA
 Na Mwandishi Maalum, New York 
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema, mafanikio ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) yatategemea uimarishishwaji wa ushirikiano kati ya Makahama hiyo na Afrika. 
Na kwa sababu hiyo, Tanzania imeshauri kuwa Rais Mpya wa Mkutano wa Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai hana budi kuhakikisha kuwa moja ya vipaumbele vyake vijielekeze katika kuimarisha uhusiano wa Makahama hiyo na Afrika. 
 Ushauri huo umetolewa na Balozi Irene Kasyanju, Mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati akizungumza katika mkutano wa kumi na tatu wa Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai. 
 Amesema Tanzania ina imani kubwa na Rais mpya wa Mkutano wa Nchi wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, Bw. Sidiki Kaba, kutoka Senegal, kuwa afanye kila awezalo katika kuimarisha uhusiano huo ambao kwa sasa umezorota. 
 Vile vile Balozi Kasyanju amesema Rais huyo anashika uongozi katika kipindi ambacho, Mahakama inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwenendo mzima wa mahakama na hasa uhusiano wake na Afrika. 
 Amebainisha kuwa, changamoto hiyo ya mahusiano na nyinginezo zinahitaji majadiliano ya uwazi yatakayowashirikisha wadau wote, na kwamba Tanzania inaamini kuwa anao uwezo huo. Akizungumzia zaidi kuhusu ushirikiano kati ya Mahakama na Afrika, Tanzania imeeleza kuwa namna ICC ilivyoshughulia shauri la Kenya hakutafanya mambo yawe shwari, kutokana na ukweli kuwa ICC ilishindwa kulifanyia kazi ombi la awali lililowasilishwa na Afrika mbele ya chombo hicho la kutaka kuahirishwa kwa shauri hilo kumechangia katika kuongeza malumbano kati ya ICC na Afrika. 
Kwa mantiki hiyo Tanzania imesema uamuzi wa hivi karibuni wa kumwondolea mashtaka Rais Uhuru Kenyata unapaswa kutoa fursa kwa mahakama hiyo kujitazama upya. Vile vile Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia fursa hiyo kumpongeza Rais Kenyatta kwa kuonyesha ushirikiano na ICC. 
Katika hatua nyingine Tanzania pia imeishauri ICC kuangalia namna itakavyoweza kufanya kazi kwa karibu na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa hasa katika kushughulikia makosa ya jinai yanayofanywa na Nchi ambazo si wanachama wa Mkataba wa Mahakama hiyo ili kuondoa dhana ya undumilakuwili katika utendaji wa ICC. 
 Tanzania imeujulisha mkutano huu kwamba ipo katika hatua yake ya awali ya kuziingiza sheria zitokanazo na Mkataba wa ICC katika mfumo wa Kisheria wa Nchi. Balozi Kasyanju anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo wa wiki mbili unaohusisha pia uchaguzi wa majaji sita wa mahakama hiyo.
 Balozi Irene Kasyanju,  Mkurugenzi wa Idara ya  Masuala ya  Sheria, Wizara ya  Mambo ya Nje na  Ushirikiano wa Kimataifa, akizungumza wakati wa   Mkutano wa  Kumi na Tatu wa  Nchi  Wanachama wa Mkataba wa  Mahakama ya  Kimataifa ya Makosa ya Jinai ( ICC). Mkutano huo wa wiki mbili  unafanyika hapa Makao  Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Sehemu ya  wajumbe wa nchi wanachama wa Mkataba wa  Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai wakimsikiliza  Mwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo, Balozi Irene Kasyanju ambaye katika hotuba yake pamoja na mambo mengine ameishauri Mahakama hiyo kuimarisha  uhusiano wake na Afrika..