Watu wawili wamefariki na mmoja kujeruhiwa katika ajali ya barabarani baada ya bus aina ya Costa kugongana na pikipiki karibu na daraja la Kileo wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro katika barabara kuu ya kutoka Moshi kwenda Dar es Salaam leo asubuhi.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema, ajali hiyo imetokea muda wa saa mbili kasoro asubuhi wakati bus hilo lenye namba za usajili T 489 CCJ lililokuwa likitoka Rombo kwenda Same kugongana na pikipiki hiyo yenye namba za usajili T398 CHT iliyokuwa ikitoka njiapanda kwenda Mwanga.
Bi Amina Mmbwambo na Bw Abdalah Shaaban, wamesema, kilio chao kikubwa ni kuwekewa bums kutokana na ajali za mara kwa mara na mwaka huu peke yake watu watatu wamepotesha maisha yao na kuiomba serikali kituo kidogo cha mabus.
Mkuu wa wilaya ya Mwanga Bw Shayibu Ndemanga amesema, dreva wa pikipiki hiyo Mohamed Ngaina ambaye ni fundi wa ujenzi alifariki papo hapo na mmoja ambaye jina lake halikufahamika amefariki wakati akikimbizwa kupelekwa hospitali ya Mawenzi na mwingine amelazwa katika hospitali hiyo.
Bw Ndemanga amesema, amewasiliana na meneja wa wakala wa barabarani mkoani Kilimanjaro Mhandisi Rubirya Marwa kuangalia uwezekano wa kujengewa bums katika eneo hilo na kituo cha bus.
Baada ya ajali hiyo wananchi wa kijiji hicho walikata mti mkubwa uliyopo kando ya barabara na kuziba barabara na kusababisha magari yakiwemo mabus ya abiria kukwama kwa zaidi ya saa tano hadi polisi walipotumia juhudi za kuuondoa kwa kutumia gari lao la mabomu ya machozi na kuruhusu magari hayo yapite saa sita na nusu mchana.