Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Ernest Mangu akimsikiliza Diwani wa Kata ya Matui Wilayani Kiteto Bw.Athuman Kidawa wakati alipofanya ziara wilayani humo kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji iliyosababisha kutokea mapigano yaliyosababisha kutokea kwa vifo.kushoto ni Afisa tarafa wa Matui Bw.Eliakimu Ndelekwa.(Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Ernest Mangu akizungumza na wananchi wa Kata ya Matui Wilayani Kiteto wakati alipofanya ziara wilayani humo kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji iliyosababisha kutokea mapigano yaliyosababisha kutokea kwa vifo. (Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Ernest Mangu akizungumza na Mtendaji wa Kijiji cha Chekanao, Kata ya Kiperesa , Wilayani Kiteto Bw.Omar Ndee (kulia) wakati alipofanya ziara wilayani humo kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji iliyosababisha kutokea mapigano yaliyosababisha kutokea kwa vifo.Katikati ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Deusdedit Nsimike pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw.Japhet Chafu (Picha na Frank Geofray-Jeshi la Polisi)
Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi, Kiteto.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Ernest Mangu ameahidi kuongeza idadi ya Askari katika kijiji cha Chekanao, kata ya Kiperesa wilayani Kiteto Mkoani Manyara kufuatia wananchi katika kijiji hicho kujitolea nyumba kwa ajili ya kuishi Askari kwa lengo la kuimarisha usalama katika maeneo yao kufuatia kuwepo kwa migogoro ya ardhi inayosababisha kutokea kwa mauaji.
IGP Mangu aliyasema hayo jana wakati alipokuwa katika ziara Wilayani Kiteto ya kujionea uharibifu uliojitokeza pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo iliyopelekea kutokea kwa vifo vya wakulima na wafugaji hivi karibuni katika wilaya hiyo ambapo watu kadhaa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na vurugu hizo.
Alisema kufuatia kuwepo kwa umbali mrefu wa kituo cha Polisi na kijiji hicho atahakikisha askari wa kudumu wanakuwepo ili kushirikiana na wananchi katika kuwabaini wahalifu wanaofanya vurugu na kuendeleza migogoro hiyo ambapo wananchi nao waliahidi kujenga kituo cha Polisi.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Chekanao Bw.Omar Ndee alisema wamekuwa wakipata shida kutokana na umbali mrefu wa kituo cha Polisi jambo ambalo limekuwa likifanya kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu vinavyochangiwa na migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kiteto.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji hicho Japhet Chafu alilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuimarisha usalama kijijini hapo tangu kutokea kwa mauji ya wakulima na wafungaji ambapo alibainisha kuwa bila kuwepo wao hali ingekuwa mbaya zaidi kutokana na kutokuwepo na muafaka baina ya wakulima na wafugaji.
"IGP hawa askari wako wasingekuwepo hapa usingekuta mtu lakini tunawashukuru sana hawa askari kwa kuwa hivi sasa hali ya usalama imerejea na hata shambani tumeanza kwenda" Alisema Bw.Chafu.
IGP Ernest Mangu alitumia ziara hiyo kuzungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, Wakaguzi wa Tarafa pamoja na Askari Kata ili kutafuta ufumbuzi wa migogoro hiyo na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama.