Friday, October 17, 2014

UHISPANIA NA UTURUKI WACHUANA VIKALI NAFASI YA UJUMBE USIO WA KUDUMU WA BARAZA KUU LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA


UHISPANIA NA UTURUKI WACHUANA VIKALI NAFASI YA UJUMBE USIO WA KUDUMU WA BARAZA KUU LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA
Na Mwandishi Maalum, New York 
Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa , jana Alhamisi waliwapigia kura ya siri wajumbe watano wasio wa kudumu watakaojiunga na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuanzia January Mosi 2015. 
 Mataifa yaliyokuwa yanawania nafasi hizo kwa kuzingatia mgawanyo wa Kikanda ni nafasi moja kutoka nchi za Afrika, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Rwanda, nafasi moja kwa kundi la nchi za Asia na Pacific ambayo kwa sasa inashikiliwa na Jamhuri ya Korea ya Kusini, nafasi moja kwa kundi la nchi za Latini ya Amerika na Visiwa vya Karibian nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Argentina na viti viwili kwaajili ya nchi za Ulaya ya Magharibi na nchi nyinginezo, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Luxembourg na Lithuania mbayo inatarajiwa kuachia nafasi hiyo mwakani ikiwa ni nafasi ya kundi la nchi za Ulaya Mashariki. 
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo Angola, New Zealand, Malaysia na Venezuela ziliibuka kidedea kwa kupita bila kupingwa huku mchuano mkali ukibakia kwa Uhispania na Uturuki. 
Kila muwania nafasi hiyo alihitaji ushindi wa theluthi mbili za wingi wa kura zilizohitajika, kura ambazo katika duru ya kwanza na ya pili ya uchaguzi kura za Uturuki na Uhispania hazikutosha na hivyo kuwalazimu kurudia kwa mara ya tatu duru ambayo Uhispania iliibuka kidedea kwa kupata kura 132. 
Wajumbe hao wataungana na wajumbe wengine watano wa kudumu wenye kura ya veto ambao ni Marekani, Urusi, Uchina, Uingereza na Ufarasa. Pamoja na wajumbe hao watano wa kudumu wajumbe wengine watakaoendelea hadi mwishoni mwa 2015 ni Chad, Chile, Jordan na Nigeria na hivyo kufanya idadi ya wajumbe wa Baraza Kuu la Usalama kuwa 15. Kumi kati yao wakiwa hawana dhamana ya kura ya Veto. 
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ndilo limekasimiwa jukumu la masuala yote yanayohusu Amani na Usalama wa Kimataifa kwa Mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, Bw. Jose Manuel Garcia Margallo akifuatillia duru ya  tatu ya Uchaguzi wa wajumbe wasio wakudumu wa  Baraza  Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa  katika uchaguzi uliofanyika siku ya Alhamisi ambapo nchi yake ilichuana vikali na  Uturuki ambapo hatimaye  Uhispania iliibuka kidedea kwa  kupata kura  132 dhiti ya Uturuki na hivyo kuungana na  Angola,  Venezuela,  New Zealand na Malayasia watakaokuwa wajumbe  wasio wa kudumu wa Baraza hilo kuanzia  Januari Mosi 2015 wakichukua nafasi za  wajumbe wanaomaliza muda wao wa miaka miwili ambao ni  Rwanda,  Jamhuri ya Korea ya Kusini, Argentina, Australia na Luxembourg. Baraza  Kuu la  Usalama la Umoja wa Mataifa ndiyo lenye dhamana ya  kusimamia masuala ya  amani na usalama wa  Jumuiya ya Kimataifa kwa mujibu wa   Katiba ya Umoja wa Mataifa.  Baraza linakuwa na wajumbe 15 ambapo watano ni wakudumu na wenye kura ya veto na kumi wasio  wakudumu  na ambao huchaguliwa kwa mgawanyo wa kikanda