Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA) Imeanza rasmi zoezi la Usajili na Utambuzi wa Watu Mkoa wa Morogoro pamoja na uchukuaji alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki kwa wananchi wa Wilaya ya Kilombero ambao zoezi la Ujazaji fomu za maombi ya vitambulisho lilishafanyika. Kuanza kwa usajili na Utambuzi wa Watu mkoa wa Morogoro kumefuatia kukamilika kwa zoezi kama hili mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara ambapo sambamba na usajili unaoendelea sasa mkoani Morogoro zoezi la uchukuaji alama za vidole picha na saini ya kielektroniki limekuwa likiendelea katika baadhi ya Wilaya za mkoa wa Pwani.
Mkoani Morogoro; katika eneo la Mikese kijiji cha Fulwe tumeshuhudia msururu wa watu wakisubiri kusajiliwa huku wengine wakiwa katika harakati za kuingizwa katika Rejesta ya Makazi inayomilikiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Vijiji. Kwa utaratibu wa sasa ili uweze kusajiliwa lazima kwanza kuwa unatambulika katika serikali yako ya Mtaa/Kijiji na kuwa umeorodheshwa katika Rejesta ya Makazi ya Mtaa au Kijiji husika.
Leo ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza kwa zoezi hilo litakalodumu kwa siku saba mpaka Jumapili ya tarehe 29/09/2014 wananchi wengi wameonekana kuhamasika na kujitokeza kwa wingi katika siku ya kwanza tofauti na mazoea ya wengi kujitokeza siku za mwisho za zoezi.
Changamoto kubwa bado imebaki wananchi wengi kukosa Viambata msingi vya kuwatambulisha kama vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya elimu ya msingi au sekondari n.k jambo ambalo limekuwa likisisitiziwa sana na NIDA katika kurahisisha utambulisho wa mwombaji. (Picha na Rose Mdami- NIDA)