Mkuu wa wilaya ya Sikonge Hanifa Selengu (aliyeshika mkoba) akikabidhi bajaj hiyo kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Vijana Simon Mang'ombe.
Vijana walioko katika Kijiji cha Mafunzo Sikonge wakifurahia chombo hicho cha usafiri kinachoendeshwa na kijana mwenzao.
Mmoja wa vijana wa Kijiji cha Mafunzo akitoa neno la shukrani mbele ya mheshimiwa DC kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Bajaj iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa 'Kijiji cha Mafunzo ya Vijana' wilayani Sikonge, mkoani Tabora.
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Kayanza Peter Pinda ametoa msaada wa bajaj kwa 'Kijiji cha Mafunzo ya Vijana' maarufu kwa jina la 'Pathfinder Green City' kilichoko wilayani Sikonge mkoani Tabora.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mkuu wa wilaya ya Sikonge Hanifa Selengu alisema bajaj hiyo imetolewa na mheshimiwa Waziri Mkuu ikiwa ni utekelezaji ahadi aliyotoa mapema mwaka jana alipotembelea kituo hicho.
Alisema chombo hicho cha usafiri ni mkombozi kwa vijana walioko kijijini hapo kwa kuwa kitawarahisishia ubebaji wa mazao na bidhaa mbalimbali wanazozalisha kutoka eneo moja kwenda jingine hasa ikizingatiwa kuwa ukubwa wa kijiji hicho ni takribani ekari 200 na uzalishaji unafanyika katika maeneo mbalimbali ya kijiji.
Aliongeza kuwa chombo hicho kitatumika pia kubebea wagonjwa kutoka kjijini hapo mpaka kwenye kituo cha afya mjini Sikonge, lakini akawatahadharisha kutokitumia kinyume na utaratibu uliowekwa kwani kufanya hivyo ni matumizi mabaya na kukiuka utaratibu jambo litakalosababisha kiharibike mapema.
Serikali ya CCM inawajali sana vijana na inatambua umuhimu wao na mchango wao katika uzalishaji mali ndio maana serikali imeruhusu kijiji hicho cha kipekee cha mafunzo kwa vijana kianzishwe wilayani humo sambamba na kutembelewa na wageni mbalimbali'aliongeza.
Akizungumzia utunzaji wa chombo hicho Selengu alisema uongozi wa kijiji ndio utakaowajibika kukitunza sambamba na kupanga jinsi kitakavyotumika katika shuguli mbalimbali za kijiji na sio za kibinafsi huku akibainisha kuwa halmashauri ya wilaya ndiye mwangalizi mkuu na itasimamia suala zima la matengenezo (servicing).
Aidha alisema kijiji hicho ambacho kinatoa mafunzo ya ujuzi mbalimbali kwa vijana wapatao 100 kwa nadharia na vitendo kimetenga maeneo tofauti tofauti kwa ajili ya shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo cha mazao mbalimbali, bustani (greenhouse), ufugaji wa kuku na ng'ombe, ufyatuaji matofali, ujenzi na ufundi.
Baadhi ya vijana walioko kijijini hapo Said Salum, Tausi Jonas na Simon Mang'ombe (Mwenyekiti wa kijiji) walimshukuru Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa msaada huo kwani walikuwa wanapata shida sana wanapotaka kusafirisha mazao na bidhaa zingine wanazozalisha toka sehemu moja kwenda nyingine katika kijiji hicho.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Richard Unambwe ambaye pia ni mwanasheria wa halmashauri hiyo aliwaasa vijana hao kukitumia vizuri chombo hicho ili kiwasaidie katika mafunzo yao sambamba na kutoa taarifa punde kinapoharibika.
Aidha Unambwe aliwahakikishia vijana hao kuwa halmashauri yake itaendelea kutoa msaada unaostahili kijijini hapo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa hususani kuwapa ujuzi mbalimbali utakaowasaidia kujiajira wenyewe punde wamalizapo mafunzo yao kijijini hapo.