Friday, August 22, 2014

WANANCHI WENGI WAJITOKEZA ZOEZI LA USAJILI NA UTAMBUZI WA WATU MKOANI MTWARA



WANANCHI WENGI WAJITOKEZA ZOEZI LA USAJILI NA UTAMBUZI WA WATU MKOANI MTWARA
Zoezi la Usajili Vitambulisho vya Taifa limeendelea mkoani Mtwara, ambapo wananchi wamejitokeza kwa wingi kujisajili, kama wakazi hawa wa Wilaya za Tandahimba na Newala walivyokutwa wakishiriki kikamilifu kujisajili.

Moja ya changamoto kubwa iliyojitokeza ni wakazi wengi hususani maeneo ya vijijini kukosa mashine za photocopy, huku baadhi wakikosa nyaraka muhimu za kuwatambulisha. Changamoto nyingine ni waombaji wengi kutokuwa na taarifa sahihi za umri wao binafsi na wazazi huku baadhi wakikosa taarifa sahihi za maeneo wanakoishi.

Hata hivyo kwa maelekezo na mafunzo yaliyotolewa na NIDA kwa maafisa wote wanaoendesha zoezi hilo changamoto nyingi zimeweza kutatuliwa kutokana na miongozo na madodoso yanayomsaidia mwombaji kutambua baadhi ya taarifa muhimu.
Hata hivyo NIDA imewaomba wananchi katika maeneo mengine ambayo zoezi hili halijafanyika kuanza kujiandaa kwa kuwa na nyaraka muhimu zinazoweza kuwatambulisha mathalani; cheti cha kuzaliwa, kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, Cheti cha Elimu ya Msingi, Sekondari au Chuo, Leseni ya Udereva, Kadi ya kupigia Kura, Pasipoti, Kadi ya Bima ya Afya, nambari ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN) pamoja na kuwa taarifa sahihi zinazomhusu mwombaji binafsi na wazazi, majina, tarehe na miaka ya kuzaliwa.