Tuesday, August 05, 2014

WAMBURA KUANIKA 'MBIVU NA MBICHI' BAADA YA KUFUKUZWA UANACHAMA SIMBA SC



WAMBURA KUANIKA 'MBIVU NA MBICHI' BAADA YA KUFUKUZWA UANACHAMA SIMBA SC
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
BAADA ya mkutano mkuu wa klabu ya Simba uliofanyika jana Agosti 3, 2014 kufikia maamuzi ya kuwafuta wanachama 72 uanachama wa klabu hiyo kwa kosa la kupeleka masuala ya mpira mahakamani, Michael Richard Wambura ataunguruma kesho kuzungumzia hilo.
Katibu mkuu huyo wa zamani wa kilichokuwa chama cha soka Tanzania, FAT ni miongoni mwa wanachama hao waliofukuzwa jana na mkutano mkuu.
Wambura na Mtemi waliipeleka Simba mahakamani mwaka 2010 kinyume na katiba ya Simba, TFF, CAF na TFF ambapo ni marufuku kupeleka masuala ya mpira katika mahakama za kawaida za haki.
Wanachama wengine 70 walienda mahakama kuu wakipinga kuenguliwa kwa Wambura katika uchaguzi wa juni 29 kwa madai kuwa katiba ya Simba imekiukwa, hivyo wakaitaka mahakama kusimamisha uchaguzi.
Mahakama ilikubali kusikiliza shauri hilo na kesi ipo mahakamani, lakini iligoma kusimamisha uchaguzi wa Simba uliofanyika juni 29 mwaka huu.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam, Wambura amasema kesho atapata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari, hivyo itakuwa nafasi nzuri ya kuweka kila kitu wazi.
"Nimesoma kwenye vyombo vya habari leo asubuhi kuwa jana kulikuwa na mkutano mkuu na ulikuwa unahusu wanachama 69 waliopeleka kesi mahakamani, pamoja na mimi na mwenzangu tuliopeleka kesi mwaka 2010." Alisema Wambura.
"Mimi natafakari na nadhani kesho nitaongea  na waandishi wa habari baada ya kuwasiliana na watu mbalimbali, kujua wanasheria wanasemaje na katiba ya Simba inasemaje. Kesho nitaeleza kwa kina kila kitu na maswali yote yatajibiwa."
Jana makamu mwenyekiti wa Simba sc, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema wanachama wote waliofukuzwa walipewa barua kabla za kuwataka wafike kwenye mkutano mkuu, lakini hakuna hata mmoja aliyehudhuria.
Lakini Wambura ameonekana kukana kupata barua hiyo na kauli yake ni hii hapa: "Kama mimi nimesoma leo kwenye vyombo vya habari kuwa kulikuwa na mkutano mkuu, unapata jibu kuwa nilipata barua au hapana. "Hivyo vyote ni suala la ushahidi, kama kweli walinipa barua,  ni nani alinipa, nani alisaini, zilikuwa barua za nini"

"Cha muhimu kesho nitazungumza na waandishi wa habari na itakuwa ni nafasi nzuri ya kueleza yote."