Friday, April 08, 2016

KITWANGA ATAKA MADAKTARI, WAUGUZI WANAOJIHUSISHA NA RUSHWA WACHUKULIWE HATUA KALI JIMBONI KWAKE.



KITWANGA ATAKA MADAKTARI, WAUGUZI WANAOJIHUSISHA NA RUSHWA WACHUKULIWE HATUA KALI JIMBONI KWAKE.
 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza, Charles Kitwanga (aliyevaa koti) akicheza ngoma ya asili na wananchi wa Kata ya Sumbugu wilayani Misungwi mara baada ya kuwasili katika eneo hilo kwa ajili ya kufungua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi hao. Waziri Kitwanga amemaliza ziara jimboni kwake leo na kuwaonya madaktari na wauguzi wilayani humo kuacha tabia ya kuwaomba rushwa wananchi. 
 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza, Charles Kitwanga akizungumza na wananchi wa Kata ya Sumbugu wilayani Misungwi. Katika hotuba yake, Kitwanga aliwataka wananchi wa jimbo lake washirikiane ili kuliletea maendeleo jimbo hilo na kuwaonya madaktari na wauguzi wilayani humo kuacha tabia ya kuwaomba rushwa wananchi. Kitwanga amemaliza ziara jimboni kwake leo.  
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza, Charles Kitwanga (katikati meza kuu) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ihelele wilayani Misungwi. Katika hotuba yake, Kitwanga aliwataka wananchi wa jimbo lake washirikiane ili kuliletea maendeleo jimbo hilo na aliwaonya madaktari na wauguzi wilayani humo kuacha tabia ya kuwaomba rushwa wananchi. Kitwanga amemaliza ziara jimboni kwake leo.  Picha zote na Felix Mwagara.
Picha na Felix Mwagara.

Na Felix Mwagara, Misungwi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza, Charles Kitwanga amemtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Misungwi kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafukuza kazi wauguzi na madaktari watakaokuwa wanawaomba rushwa wananchi jimboni kwake.

Kitwanga alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwa muda mrefu kuwa rushwa imekithiri katika hospitali ya Wilaya jimboni humo na kuwakatisha tamaa wananchi wanaoenda kupata huduma hospitalini hapo.

Akizungumza huku akishangiliwa na mamia ya wananchi wa mjini Misungwi, Kitwanga alisema hali sasa imekuwa tete hivyo lazima tuchukue hatua kali kwa wale watumishi wachache ambao hawafuati sheria na kuweka mbele rushwa kwa wananchi.

"Ndugu wananchi madaktari na wauguzi ni watu muhimu sana katika jamii kwani wanatupa huduma nzuri kabisa, ila wataalamu hawa wanachafuliwa majina yao kwa watumishi wachache mno, sasa tunataka kuwaondoa wale wachache ili tubaki na wengi ambao wanaipenda kazi yao, nawaonya wale wachache wenye tabia hiyo waiache haraka iwezekanavyo," alisema Kitwanga.

Alifafanua kuwa ni kosa kwa daktari au muuguzi kumuomba rushwa mgonjwa au ndugu wa mgonjwa, kufanya hivyo ni hatari ni sawa na kuua, hivyo lazima sheria ifuate mkondo wake ili kulimaliza tatizo hilo sugu ndani ya Hospitali ya Wilaya pamoja na Misungwi kiujumla.

"Ndugu wananchi msiwe na wasiwasi kabisa, nina aapa sitalivumilia tatizo hilo, na Mkurugenzi yupo hapa analisikia hili, hivyo lazima alifanyie kazi kwa kuwasimamisha kazi wauguzi au madaktari watakaotuhumiwa kuomba au kupokea rushwa," a;lisema Kitwanga huku akishangiliwa na wananchi jimboni humo.   

Wakati huohuo, Kitwanga aliwataka wananchi hao kuanzisha vikundi ili waweze kupewa mikopo kupitia fedha alizoziahidi Rais John Magufuli kuwa atatoa kwa kila kijiji shilingi milioni hamsini.
"Fedha zipo jirani kuja, hivyo anzisheni vikundi ili muweze kukopeshwa fedha hizo na muweze kufanya mambo ya maendeleo, fedha hizo ni kwa ajili ya mikopo hivyo tumieni fursa hiyo kwa kuanzisha vikundi vyenu ili muweze kuzipata fedha hizo kwa uharaka zaidi," alisema Kitwanga.

Hata hivyo, Waziri Kitwanga aliwahakikishia wananchi wa jimbo hilo wawe watulivu na wasubiri maendeleo, na pia waendelea kuchangia maendeleo ya jimbo lao ikiwemo uchangiaji wa madawati katika shule zao. Kuhusu barabara Kitwanga alisema barabara zote ambazo hazipitiki zitatengenezwa hivi karibuni na tatizo la maji litakuwa historia kwani mipango ya upatikanaji wa maji hayo ilishakamilika.